M23 wasitisha mapigano DRC | Mwananchi

Mwanza. Muungano wa makundi ya waasi ya AFC na M23, umetangaza kusitisha mapigano nchini humo kwa kile ambacho umedai ni uwepo wa janga la kibinadamu linalolikumba taifa hilo.

Taarifa iliyotolewa na Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), jana Jumatatu Februari 3,2025, imesema:

“Muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), unautangazia umma kuwa kwa kuzingatia janga la kibinadamu lililosababishwa na utawala wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), tumesitisha mapigano kuanzia leo Februari 4,2025, kwa sababu za kibinadamu.”

Taarifa hiyo imeenda mbali na kulishutumu Jeshi la Ulinzi la DRC la FARDC, kwa kutumia ndege za kijeshi kutekeleza mashambulizi yaliyosababisha mauaji ya wapiganaji wake karibia na uwanja wa ndege wa Kavumu nchini humo.

“Ifahamike kuwa hatuna lengo la kuuteka Mji wa Bukavu ama maeneo memgine. Hata hivyo, tunalenga kupigania na kulinda maslahi ya raia wa DRC,” imesema taarifa.

Umesema: “Tunaitaka SAMIDRC, kuondoa vikosi vyake nchini DRC, kwa sababu lengo ambalo lilisababisha walinda amani hao kuwepo nchini DRC limeshatoweka.”

Waasi wa kundi la M23, walianza operesheni yao ya kuitwaa miji ya Mashariki wa DRC hususan Mji wa Goma uliopo katika Jimbo la Kivu Kaskazini mwishoni mwa mwezi Januari 2025, kisha kutangaza kujitanua na kuahidi kufanya maandamano hadi Mji Mkuu wa Taifa hilo wa Kinshasa.

Kabla ya kutolewa taarifa hiyo ya kusitisha mapigano, Kiongozi wa muungano wa makundi ya waasi, likiwemo la M23, Corneille Nangaa lengo lao lilikuwa ni kuung’oa utawala wa Rais Felix Tshisekedi madarakani na kuuweka utawala mpya.

Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts