Dar es Salaam. Miaka 27 iliyopita Bill Gates na mkewe wa zamani Melinda, walizuru Tanzania kwa shughuli za utalii. Ziara hiyo iliyofanyika mwaka 1998 ilikuwa na matokeo chanya kwa nchi baada ya wawili hao kuamua kuwekeza rasilimali fedha kusaidia sekta ya afya.
Hayo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Taasisi ya Gates Foundation Kanda ya Afrika Mashariki, Samburu Wa-Shiko kutoka ofisi ya Nairobi, Kenya aliyefanya mahojiano na waandishi wa Mwananchi wiki iliyopita.
Samburu anayesimamia miradi ya Gates iliyopo Kenya, Tanzania, Rwanda, Uganda na mataifa mengine ya Afrika Mashariki, pia ameeleza sababu ya taasisi hiyo kumpa tuzo ya heshima Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Amesema tuzo hiyo ‘The Gates Goalkeepers Award’ ni kielelezo cha matokeo ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 80 kutoka vifo 556 mwaka 2016/2017 mpaka 104 mwaka 2022, kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) ya mwaka 2022.
Samburu pia ameeleza mafanikio yaliyopatikana miaka 25 tangu taasisi hiyo ianze kufanya kazi Tanzania na mwelekeo wa ufadhili kwa miaka 25 ijayo kama ifuatavyo:
Swali: Gates Foundation inafikisha miaka 25 tangu ilipoanza shughuli zake Tanzania, mahusiano kati ya pande hizi mbili yalianzaje?
Samburu: Taasisi ya Gates Foundation ilianzishwa Tanzania baada ya Bill na Melinda kusafiri Tanzania, walisoma ripoti fulani iliyoonyesha kila mwaka watoto zaidi ya nusu milioni wanafariki dunia kwa magonjwa yanayotambulika na yenye tiba na kinga.
Ni kitu kilichowaghadhabisha, waliporudi nyumbani Marekani, walikusanya wataalamu wa afya wakauliza inawezekanaje sisi tulio Marekani na nchi zilizoendelea watoto wanazaliwa wanapitia maisha mazuri na kuna ripoti zinaonyesha watoto wanapoteza maisha.
Ndipo ikagunduliwa kuwa chanzo kikuu cha vifo ilikuwa ukosefu wa tiba na kinga, hasa chanjo kwa watoto.
Uhusiano na Tanzania ulianza hivyo, kwa miaka yote hii 25, Gates Foundation imekuwa ikizingatia masuala ya afya na ubunifu kwenye chanjo, kwa sababu chanjo ina nafasi kubwa katika kulinda watoto kwenye magonjwa, hivyo kuhakikisha idadi ya vifo inapungua.
Swali: Katika miaka 25 ya utendaji kazi, ni mafanikio gani Gates inajivunia?
Samburu: Lazima tutambue mafanikio tunayoyaona Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla ni matarajio ya Gates, ambayo hutoa ufadhili pale Serikali husika inapoonyesha utayari wa kufanya kazi. Gates hutoa ufadhili kusaidia kusukuma gurudumu, hivyo pongezi zinaenda kwa Serikali.
Tanzania imefanya kazi kubwa kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya. Tumeanza kuona matokeo yanayoridhisha hasa katika afya ya kinamama, watoto na lishe bora.
Katika afya ya mama na mtoto, tumeona vifo vya kinamama vya uzazi vimepungua kwa kiasi kikubwa, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vinazidi kupungua kwa kasi.
Changamoto tulizokuwa tukiziona kama vile udumavu, utapiamlo na upungufu wa virutubisho zinaanza kupungua. Haya ni maeneo kwenye sekta ya afya, tumeona michakato ambayo inaleta maendeleo.
Swali: Nini lengo la uwepo wa Taasisi ya Gates nchini Tanzania?
Samburu: Uwepo wetu Tanzania una malengo matatu. Kwanza, ni kwa sababu mwaka 2024 Rais Samia alichaguliwa kama kiongozi wa dunia kutuzwa tuzo ya ‘The Gates Goalkeepers Award’.
Hii ni tuzo kutokana na kazi kubwa ambayo Tanzania imeifanya, ambayo pia Rais amefanya kwa kuboresha sekta ya afya hasa kwenye afya ya kinamama na watoto. Pia kupambana na changamoto ya utapiamlo.
Tumekuja kumkabidhi Rais tuzo ya Golkeeper Award 2024. Rais ilikuwa akabidhiwe tuzo mwaka jana Marekani, katika mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA) lakini kwa bahati mbaya Rais hakuja New York. Ikabidi tutoe ahadi kuwa tutakuja Tanzania kumkabidhi. Kwa hiyo, lengo la kwanza ilikuwa kumkabidhi tuzo.
Pili, tupo Tanzania pamoja na viongozi wetu akiwemo Rais wa Gates anayehusika na masuala ya usawa wa kijinsia, Dk Anita Zaidi kwa ajili ya kuboresha na kuendeleza mahusiano kati yetu na Serikali ya Tanzania.
Hatua hii inalenga kuendeleza ushirikiano na Serikali na mashirika mengine Tanzania ili kuongeza jitihada katika sekta za afya, kilimo na usawa wa jinsia, ambazo Gates inafanyia kazi.
Tuko hapa kama sehemu ya kusherehekea miaka 25 tangu kuanzishwa Gates Foundation Tanzania. Tutajadiliana na Serikali na wadau wengine kuhusu miaka 25 ijayo.
Swali: Kwa miaka 25 mmefanya kazi katika sekta ya afya, usawa wa kijinsia na mabadiliko ya tabianchi. Ni maeneo gani mengine mtaongeza nguvu nchini Tanzania?
Samburu: Kwa miaka 25 ijayo suala la afya litaendelea kuwa kipaumbele cha Gates Foundation, hasa kusaidia ubunifu katika kutafuta njia ya kupunguza kwa kasi vifo vya watoto chini ya miaka mitano.
Ufadhili tunaotoa unasisitiza ubunifu na utafiti, msisitizo utakuwa huko zaidi. Sekta ya kilimo tunajitahidi kuongeza tija, kutumia njia mbadala za kusaidia wakulima wadogo kuongeza uzalishaji na mapato. Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri tija kwa wakulima.
Katika Bara la Afrika wanaoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi ni wakulima wadogo.
Kuhusu usawa wa kijinsia, tutawezesha kinamama kupata nafasi za kufanya biashara na kuwaunganisha na masoko.
Kwa wanaojihusisha na kilimo ni muhimu kuhakikisha mazao yanafika kwenye masoko ya Tanzania na nje.
Swali: Mbali ya Tanzania, hali ikoje kwa nchi zingine mnazohudumia?
Samburu: Kuna hatua kubwa zanapigwa, mfano Rwanda kuna mifumo mingi ya kidijitali hasa katika sekta ya afya.
Kumejengwa vituo vingi vya afya tangu mwaka 1999 mpaka sasa, kina mama na watoto wanapata huduma na kuhakikisha wanajifungulia kwenye vituo, hivyo kuepuka changamoto zinazoweza kuwapata.
Swali: Una mapendekezo gani kwa Serikali ya Tanzania kwa miaka mitano ijayo?
Samburu: Naipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia kwa maendeleo tuliyoyaona, bila utashi wa kiasiasa na Serikali kutoa maamuzi ya kuwekeza kwenye sekta hizi za kipaumbele ni ngumu kuona maendeleo.
Gates Foundation linafanya kazi barani Afrika na dunia nzima, katika sekta ya afya hasa afya ya kina mama, watoto na masuala ya lishe hatujaona nchi imepiga hatua ikilinganishwa na iliyopigwa Tanzania.
Ni muhimu kukumbuka kuwa hatujafika kileleni, hivyo kuna haja ya kuendeleza hatua iliyofikiwa ili kuongeza asilimia ya uwekezaji kwenye sekta ya afya kutoka asilimia saba au nane mpaka asilimia 15 ili kufanikisha makubaliano ya Abuja.
Tunatoa wito kwa Serikali ya Tanzania ifike asilimia 15.
Hatua kubwa imepigwa kwenye ujenzi wa vituo vya afya. Tumetembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), tumevutiwa na kazi inayoendelea pale chini ya Profesa Mohammed Janabi.
Swali: Kuna mjadala kuhusu bima ya afya kwa wote unaendelea nchini, je, kuna mpango wowote maalumu kuhakikisha mnashirikiana na Tanzania kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo?
Samburu: Mjadala unaoendelea Tanzania umekuwepo pia katika maeneo mengine ya Bara la Afrika, jirani Kenya wanaendelea na mjadala huu. Rwanda, Afrika Kusini, Nigeria na kwingineko Afrika. Ni mjadala mkubwa kwa sababu nchi nyingi za Afrika kwa sasa zinapitia wakati mgumu kiuchumi na ukosefu wa fedha. Nchi nyingi zimejikuta kwenye hali ngumu kwa sababu ya madeni makubwa ambayo wakati mwingine zinashindwa kuyalipa au zikilipa kunakuwa hakuna fedha za kutosha kwenye sekta kama vile elimu, kilimo au afya.
Kwa hiyo, Gates Foundation linashirikiana na Serikali katika utafiti unaoonyesha ukiwekeza kwenye sekta ya afya unahitaji matokeo gani na elimu ili kuboresha uchumi wa nchi.
Huu ni utafiti tumeufanya kimataifa na Tanzania kuhakikisha utaalamu huu na utafiti unapatikana kupitia Wizara ya Afya.