Dar es Salaam. Wizara ya Afya nchini Tanzania imetaja aina saba za saratani zinazowasumbua wanaume na wanawake, huku ikiainisha namna ya kuepuka vihatarishi vya ugonjwa huo.
Saratani hizo ni mlango wa kizazi ikiathiri wanawake kwa asilimia 26.4, matiti asilimia 12, tezi dume asilimia tisa, koo asilimia 6.7 na utumbo mpana asilimia sita.
Takwimu hizo zimetajwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Nassoro Mzee katika maadhimisho ya Siku ya Saratani yaliyofanyika Taaaisi ya Saratani Ocean Road (ORCI) leo Februari 4, 2025.
Dk Mzee amesema zipo saratani zilizoonekana kuwaathiri zaidi wanaume na wanawake, akinukuu takwimu za Taifa za miaka mitano 2019-2023. Kupitia takwimu hizo, Dk Mzee amesema kwa wanaume wanaathiriwa zaidi na saratani ya tezi dume kwa asilimia 15.
“Pia, ipo saratani ya utumbo wa chakula kwa asilimia 14, utumbo mdogo asilimia 13, saratani ya ini asilimia tisa na saratani ya kichwa na shingo asilimia nane.
“Kwa upande wa wanawake, wanaathiriwa zaidi na saratani ya mlango wa kizazi, matiti, utumbo, koo, kichwa na shingo,” amesema.
Dk Mzee amesema ili kujikinga na saratani na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu jamii kuzingatia ulaji unaofaa ikiwamo kula matunda na mbogamboga kwa wigi.
“Vilevile kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi na chumvi, kuepuka vinywaji vyenye sukari nyingi, kufanya mazoezi na kuepuka matumizi ya bidhaa za tumbaku,” amesema.
Mbali na hayo kuhusu saratani ya mlango wa kizazi, Dk Mzee amesisitiza wasichana chini ya miaka 18 kulindwa kwa kupatiwa chanjo ya HPV.
Amesema wasichana wengi wamekuwa wakipata chanjo, hivyo matarajio ugonjwa huo utapungua kwa miaka ijayo nchini.
Kuhusu dhana potofu matumizi ya chanjo kwamba ina madhara, Dk Mzee amesema Serikali haiwezi kuruhusu vitu vyeye madhara hivyo wazazi wawaruhusu watoto wao kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.
Dk Mzee amesema taarifa ya Mfuko wa Dunia (Global fund) ya mwaka 2020 inaonyesha, Tanzania kuna watu 40,464 wanaogundulika na saratani kila mwaka nhuku vifo vikitokea 26,000.
Ameeleza kuwa, athari za saratani zimekuwa zikiongezeka na takwimu za Wizara ya Afya zinaonyesha mwaka 2018, kati ya watu sita wanaofariki dunia, mmoja wao ni kutokana na saratani.
Hadi kufikia mwaka 2030, Dk Mzee amesema athari za saratai zitakuwa zimeongezeka mara mbili kwa nchi zenye kipato cha chini.
“Ni muhimu sana kuchukua tahadhari ya ugonjwa huu, Septemba 2022 takwimu zilionyesha kusini mwa Jangwa la Sahara watu wapo kwenye hatari ya kupata saratani na kutakuwa na idadi kubwa ya vifo,” amesema.
Mtaalamu huyo ameeleza kuwa, mwaka 2030 kunatarajiwa vifo vitokanavyo na saratani vitaongezeka kufikia takribani milioni moja kutoka vifo 520,000 kwa mwaka.
Nchi za Afrika Mashariki zina idadi kubwa ya wagonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi ikilinganishwa na nchi zingine duniani.
Awali, akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Saratani ambayo hufanyika kila mwaka, Dk Mzee amesema kauli mbiu ya mwaka huu ya: “Tuungane kwa tofauti zetu,” inaaminisha jamii iungane na kumwona mgonjwa wa saratani kama binadamu na sio kuangalia ugonjwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Diwani Msemo amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye taasisi hiyo kuanzia vifaatiba hadi majengo, lengo likiwa kumhakikisha mgonjwa huduma bora za matibabu.