Mbowe, Wenje wakacha ‘fungate’ ya Chadema, Boni Yai na Sugu wamo

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimehitimisha kikao chake cha kupanga mikakati mbalimbali ikiwamo utekelezaji wa kushinikiza mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi kabla ya kuushiriki.

Oktoba 2025, Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu wa kuwachagua, madiwani, wabunge na Rais.

Kikao hicho cha Retreat ‘fungate’ kilianza Januari 30 hadi leo Jumanne, Februari 4, 2025 Bagamoyo mkoani Pwani chini ya uenyekiti wa Tundu Lissu.

Kikao hicho kimefanyika baada ya Chadema kumaliza uchaguzi wake wa ndani wa mabaraza ya wanawake (Bawacha), vijana (Bavicha) na  wazee (Bazecha) na ule wa uenyekiti ngazi ya Taifa ambao Lissu aliibuka mshindi dhidi ya Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea nafasi hiyo.

Lengo la fungate hiyo ni kuweka mikakati ya jinsi ya kutekeleza msimamo wao wa ‘No reform no election,’ na kutibu majareha yaliyotokana na uchaguzi huo wa ndani.

Katika Kikao hicho, Mbowe ambaye ni mjumbe wa kudumu wa kamati kuu na Ezekia Wenje ambaye ni Mwenyekiti wa Kanda ya Viktoria hawakuwa miongoni mwa walioshiriki Kikao hicho.

Katika uchaguzi huo, Wenje alikuwa mgombea wa makamu mwenyekiti bara akimuunga mkono Mbowe naye alishindwa na John Heche aliyekuwa akimuunga mkono Lissu.

Kabla na baada ya uchaguzi huo ulishuhudia minyukano ya kambi mbili zilizokuwa zikiwaunga mkono Mbowe na Lissu. Licha ya Mbowe kukubali matokeo na kuwataka wote kuwa wamoja kama kauli mbiu yao ya ‘Strong Together’ bado kumekuwapo na minyukano ya chini kwa chini kwenye makundi kijamii.

Mwananchi limemtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, Apollo Boniface kujua ushiriki wa Mbowe na Wenje kwenye Kikao hicho ambapo amekiri wawili hao hawajashiriki.

“Kikao kilichokuwa kinafanyika Bagamoyo kimeisha leo, lakini Mbowe na Wenje hawajashiriki na sababu za kutokushiriki kwao bado hazijajulikana bado tunasubiri,” amesema.

Hata hivyo, Mwananchi limemtafuta Wenje na Mbowe kwa simu zao za mkononi kujua kwa nini hawakushiriki hawakupatikana na jitihada za kuwasaka zinaendelea.

Januari 29, 2025, baada ya kuripoti kwa mara ya kwanza kwenye ofisi za chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam, Lissu aliwataka wanachama na viongozi wote kuungana kukijenga chama chao na kuepuka migawanyiko.

Lissu alisema uchaguzi mkuu wa chama hicho uliokwisha ulikuwa wa kihistoria na kuwezesha uongozi wao kukabidhiwa ofisi kwa amani.

“Kwa sababu ya uchaguzi wenyewe ulileta maneno mengi sana, tumevutana sana, tumesemana sana, mara nyingi hatukusifiana, tumezungumza yaliyo mabaya yetu.

“Sasa uchaguzi umepita, hiyo sababu iliyotufanya tuvutane imepita na imepita kwa namna ambayo nchi nzima inatusifia.

“Kwa hiyo kwa sababu tumefanya jambo la kihistoria, bado tuna sababu ya kuendelea kuvutana? Kunyoosheana vidole,” amehoji.

 “Tunarudi nyumbani, wote ni wa nyumba moja, palipobomoka tupajenge, palipopasuka tuparudishe wote. Tumeshinda wote, sasa huyu mtoto tumlee wote kwa sababu ni mtoto wetu. Tusikubali maneno ya “haya tutaona watafanyaje kazi.” Wote ni wa nyumba moja,” amesema.

Huku akirejelea hotuba ya aliyekuwa Rais wa Marekani, Abraham Lincoln aliyoitoa Machi 4, 1964 baada ya kushindwa urais, huku majimbo manne ya nchi hiyo yakijitenga naye na kuanzisha vita.

“Kwenye uapisho akahutubia akasema, “hatupaswi kuwa maadui, japokuwa yapo yaliyotuumiza, yanayotuunganisha yana nguvu kuliko yanatotutenganisha.”

Kuhusu mabadiliko wanayopigania, Lissu alisema: “Mimi ninaamini na nina ushahidi wa kutosha wa chaguzi tatu zilizopita zinaunga mkono kauli ya ‘No reforms, no election’ (Hakuna Mabadiliko, Hakuna uchaguzi).

“Tukisema hivyo tunazungumzia njia za kushurutisha mageuzi, si njia ya kawaida kwenda kuwaomba walete mageuzi. ndivyo walivyofanya Kenya, Malawi na Zambia,” amesema Lissu alipoulizwa swali kuhusu kaulimbiu yao ya ‘No reforms, no election.’

Akieleza mpango wa viongozi wa chama hicho kujifungia wiki nzima kupanga mikakati, Katibu Mkuu, John Mnyika alisema: “Mwaka huu ni wa reforms (mabadiliko), Mwenyekiti atatuongoza. Reforms hizi ni kuongoza nguvu za pamoja, baada ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tulitafakati kwenye mkutano mkuu tukatoka na maazimio, yakapelekwa kamati kuu.”

Alisema moja ya maazimio ni kutaka kuwa na mabadiliko ya Katiba ya kuwa na mfumo mpya wa chaguzi ikiwamo kauli ya ‘No reforms no election.’

Alisema kutokana na kazi nzito iliyo mbele yao, hawatarajii kuona migawanyiko ndani ya chama.

“Katika wakati huu ambao tunatafuta Reforms za kikanuni na kikatiba, hatupaswi kuendeleza tofauti zetu za kiuchaguzi. Stronger together (nguvu kwa pamoja),” alisema.

Related Posts