Mbunge CCM ahoji utekelezaji wa ahadi za viongozi

Dodoma.  Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka amehoji Serikali inatumia utaratibu gani kuhakikisha utekelezaji wa ahadi za viongozi wakuu unafanyika ili zisionekane kama ahadi zisizotekelezeka.

Kuchauka amesema hayo bungeni leo Jumanne, Februari 4, 2025, katika kipindi cha maswali na majibu.

Suala la utekelezaji wa ahadi za viongozi liliwahi kujadiliwa Mei 2021, wakati wa mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka 2021/2022 huku wabunge wakieleza wasiwasi wao kuhusu ahadi za marais waliopita, Benjamin Mkapa (marehemu), Jakaya Kikwete na John Magufuli (marehemu).

Pia, katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya mwaka 2023/2024, mbunge wa Sengerema (CCM), Hamis Tabasamu alilalamikia ucheleweshaji wa utekelezaji wa ahadi hizo, akisema zinawatesa wananchi.

Akijibu swali hilo leo, Naibu Waziri wa Nchi (Ofisi ya Waziri Mkuu) Sera, Bunge na Uratibu, Ummy Nderiananga amesema Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ina jukumu la kuratibu utekelezaji wa ahadi zinazotolewa na viongozi wakuu wa kitaifa.

Amesema uratibu huo unafanyika wakati viongozi hao wanaposhiriki katika matukio mbalimbali ya kitaifa ikiwamo mikutano na kampeni za uchaguzi mkuu.

“Mara baada ya viongozi hao kutoa ahadi/maagizo ofisi binafsi za viongozi hao kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu huziwasilisha kwenye wizara za kisekta kwa ajili ya utekelezaji na kutoa mrejesho,” amesema.

Amesema ili kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa ahadi hizo zinazowasilishwa zinakua na uhalisia, Ofisi ya Waziri Mkuu ilibuni na kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Uratibu na Ufuatiliaji wa Shughuli za Serikali (Dashboard).

Amesema mfumo huo umeimarisha uratibu na ufuatiliaji wa ahadi hizo, kuweka kumbukumbu za ahadi hizo na kuwawezesha wataalamu kutumia muda mfupi kutuma maelekezo na kupokea taarifa za utekelezaji kutoka kwenye wizara na sekta husika.

Katika maswali ya nyongeza, Kuchauka amehoji kwa nini Serikali isiweke katika bajeti utekelezaji wa ahadi hizo ili wabunge waweze kuzifuatilia pale  bajeti hiyo inapoachwa kutekelezwa.

“Kule kwangu Barabara ya Nangurukulu –Liwale  na Barabara Nachingwea-Liwale ni miongoni mwa ahadi za uchaguzi 2015 na 2020, je nini kauli ya Serikali juu ya utekelezaji wa ahadi hizo,”amehoji.

Akijibu maswali hayo, Ndeliananga amesema katika wizara ya kisekta, ahadi za viongozi ni kipaumbele chao, hivyo wamekuwa wakiweka kila wanapowasilisha bajeti zao.

“Na sisi Ofisi ya Waziri Mkuu tunafanya kazi ya kuratibu kuhakikisha ahadi hizi zimewekwa katika bajeti na kuwa katika Dashbord tunaona imefikia wapi na utekelezaji umefikia asilimia ngapi kwenye kila sekta,” amesema.

Kuhusu barabara za jimbo hilo, amesema Halmashauri ya Liwale kupitia Ofisi ya Tamisemi mwaka jana ilitoa fedha kwa maafa yaliyotokea kwenye El-Nino na Kimbunga cha Hidaya Sh1.3 bilioni ili kuendelea kutengeneza barabara hizo.

“Lakini bajeti yako mheshimiwa Kuchauka imeongezeka kutoka Sh839 milioni hadi Sh1.4 bilioni hadi tunavyoongea leo, nataka nikuhakikishie ahadi zote za viongozi wakuu tunaendelea kuzifanyia kazi. Tunataka Watanzania watuamini na waamini Serikali ya awamu ya sita kwa sababu ahadi zote ni vipaumbele vya Serikali,” amesema.

Related Posts