Mvua kubwa, upepo mkali kuanzia leo

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri uwepo wa mvua kubwa na hali mbaya ya hewa katika mikoa tisa nchini, hali inayotarajiwa kudumu kwa siku tano kuanzia leo Jumanne hadi Jumamosi

Mvua hizo zitanyesha kuanzia leo katika mikoa ya Rukwa, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara, Morogoro na Mbeya.

Mamlaka hiyo pia, imeonya uwepo wa upepo mkali wa kilomita 40 kwa saa ukanda wa Pwani wa Bahari ya Hindi, mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Mtwara, Mafia Lindi pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

Taarifa iliyotolewa leo Februari 4, 2025 na TMA imeonesha hali mbaya ya hewa itaanza leo Jumanne katika mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Athari zinazoweza kujitokeza ni kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi, uvuvi na usafirishaji baharini,” inaeleza taarifa hiyo.

Kwa Februari 5, mamlaka hiyo inaeleza kuwa maeneo machache ya mikoa ya Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Mkoa wa Morogoro yatapata mvua kubwa.

Angalizo la upepo mkali wa kilomita 40 kwa saa na mawimbi yanayofikia mita mbili limetolewa katika maeneo ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara pamoja na Unguja na Pemba.

Kwa Februari 6, 2025 TMA imetoa angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili.

Tahadhari hiyo ni kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi katika mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi, Mtwara, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Athari zinazoweza kujitokeza ni kuathirika kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi ukiwamo uvuvi na usafirishaji baharini,” inaeleza taarifa hiyo.

Related Posts