KUNA mshtuko umetokea leo jioni kwenye mazoezi ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wakati kikosi hicho kikijiandaa na mchezo wa ligi hiyo utakaochezwa kesho Jumatano Februari 5, 2025 dhidi ya KenGold utakaochezwa Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Unavyosoma taarifa hii ni kwamba kocha wa Yanga, Sead Ramovic atamalizia mchezo huo wa kesho dhidi ya KenGold kisha atatimka rasmi ndani ya klabu hiyo.
Kuondoka kwa Ramovic kunaelezwa ni baada ya kocha huyo kupata dili la maana kutoka kwa Waarabu wa Algeria.
Waarabu hao si wengine bali ni CR Belouizdad ndio inayomng’oa Ramovic ndani ya Yanga baada ya kumpa dili la maana kwenda kuchukua nafasi ya kocha Abdelkader Amrani aliyeachana na timu hiyo Januari 25, mwaka huu.
Kabla ya Ramovic hajatua CR Belouizdad, timu hiyo kwa sasa inanolewa na Samir Houhou akiwa kaimu kocha mkuu.
Ramovic atakapomaliza kuiongoza Yanga kwenye mchezo wa kesho dhidi ya KenGold atakuwa amefikisha siku 81 ndani ya klabu hiyo tangu apewe kibarua hicho Novemba 15, 2024 akichukua nafasi ya Muargentina Miguel Gamondi.
Ishu ipo hivi; Kikosi cha Yanga kilikiwa mazoezini leo jioni kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KenGold utakaochezwa leo Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam ambapo Ramovic aliwashtua wachezaji akiwaaga rasmi kwamba baada ya mchezo huo hataendelea kuwa kocha wa timu hiyo hatua ambayo iliwachanganya wengi.
“Ni kweli kocha ametuaga baada ya mazoezi kumalizika, kwakweli imetushtua sana, kwanza tulidhani labda amegombana na uongozi lakini ameweka wazi kwamba amepata nafasi ya kwenda kufanya kazi sehemu nyingine,” alisema mmoja wa mastaa wa timu hiyo.
“Unajua alishaanza kukaa kwenye mioyo yetu, imekuwa ghafla sana kuondoka kwake na unajua bora tungesikia kwanza tetesi lakini amtusapraizi tu baada ya mazoezi na kutuaga.”
Katika ujumbe wake Ramovic amewataka wachezaji wa Yanga kupigania pointi tatu za kesho lakini pia kuhakikisha timu yao inakwenda kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Kocha huyo ameiongoza Yanga kwenye jumla ya michezo 13 ya mashindano yote ikiwemo sita ya Ligi Kuu Bara aliyoshinda yote, sita Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi akishinda miwili, sare mbili na kupoteza mbili, pia mchezo mmoja wa Kombe la Shirikisho (FA) akishinda pia.
Ramovic mpaka anaondoka Yanga alifanikiwa kuongoza msimamo wa ligi kwa saa zisizozidi 24 kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Kagera Sugar akiishusha Simba kabla ya wekundu hao kumshusha siku inayofuata ilipoichapa Tabora United kwa mabao 3-0.
Ingawa hakuna kiongozi wa Yanga aliyekubali kueleza taarifa hiyo lakini Ramovic ameshawadokeza mabosi wa juu kabisa wa klabu hiyo juu ya uamuzi wake huo wa kuondoka mara baada ya mchezo wa kesho.
Ramovic kutua kwake CR Belouizdad, atakuwa amemnyima ulaji kocha wa zamani wa Simba Abdelhak Benchikha aliyekuwa kwenye mazungumzo na klabu hiyo kwa takribani wiki moja sasa baada ya kuachana na JS Kabylie.
Wakati Ramovic akiondoka Yanga, nafasi yake inachukuliwa na Abdihamid Moallin ambaye alitambulishwa kikosini hapo Novemba 18, 2024 kama Mkurugenzi wa Ufundi akitokea KMC alipokuwa kocha mkuu.
Hii itakuwa ni timu ya tatu Moallin kuiongoza kama kocha mkuu baada ya kufanya hivyo akiwa Azam kuanzia Julai 2021 hadi Agosti 2022, kisha Julai 2023 hadi Novemba 2024 akiinoa KMC.
MECHI ALIZOONGOZA RAMOVIC YANGA
Ligi Kuu Bara: 06
Ushindi: 06
Sare: 00
Kupoteza: 00
Mabao ya kufunga: 22
Mabao ya kufungwa: 02
Kombe la FA: 01
Ushindi: 01
Sare: 00
Kupoteza: 00
Mabao ya kufunga: 05
Mabao ya kufungwa: 00
Ligi ya Mabingwa: 06
Ushindi: 02
Sare: 02
Kupoteza: 02
Mabao ya kufunga: 05
Mabao ya kufungwa: 06
JUMLA:
Mechi: 13
Ushindi: 09
Sare: 02
Kupoteza: 02
Mabao ya kufunga: 32
Mabao ya kufungwa: 08
MATOKEO RAMOVIC AKIWA YANGA
Yanga 0-2 Al Hilal
Namungo 0-2 Yanga
MC Alger 2-0 Yanga
TP Mazembe 1-1 Yanga
Yanga 3-2 Mashujaa
Yanga 4-0 Tanzania Prisons
Dodoma Jiji 0-4 Yanga
Yanga 5-0 Fountain Gate
Yanga 3-1 TP Mazembe
Al Hilal 0-1 Yanga
Yanga 0-0 MC Alger
Yanga 5-0 Copco
Yanga 4-0 Kagera Sugar