Dar es Salaam. Mkutano wa marais wa nchi wanachama za Jumuiya ya Maendeleo ya kusini mwa Afrika (Sadc) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), unatarajiwa kuwakutunaisha Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Pia, mkutano huo utamkutanisha Rais Kagame na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, ambapo awali walirushiana vita vya maneno.
Mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili Ijumaa na Jumamosi, ukianza na mkutano wa mawaziri na baadaye mkutano wa marais.
Ajenda kuu ya mkutano huo ni mapigano yanayoendelea Goma, DRC kati ya majeshi ya M23 na majeshi ya Serikali ya DRC, huku pia kukiwa na majeshi ya kulinda amani ya Umoja wa Mataifa na yale ya SADC.
Taarifa ya mkutano huo ilitolewa na Mwenyekiti wa EAC, Rais wa Kenya William Ruto, unafanyika baada ya maazimio ya mikutano miwili ya dharura ya marais kuomba kufanya mkutano wa pamoja.
Rais Kagame atahudhuria kwa kivuli cha uanachama wake EAC, huku Tshisekedi nchi yake ni mwanachama wa jumuiya zote za EAC na Sadc huku Ramaphosa nchi yake ikiwa ni mwanachama wa Sadc.
Rais Kagame alihudhuria mkutano wa dharura wa EAC uliofanyika Nairobi, nchini Kenya, Rais Tshisekedi licha ya kuwa mwanachama alisusa kuhudhuria mkutano huo na alihudhuria wa Sadc ambao ulihudhuriwa pia na Ramaphosa.
Hata hivyo, kwa upande wa Rais Tshisekedi ambaye nchi yake ni mwanachama wa jumuyia zote mbili EAC na Sadc, hakuhudhuria mkutano wa dharura wa EAC, lakini alihudhuria mkutano wa dharura wa marais wa Sadc uliofanyika Harare nchini Zimbabwe.
Maazimio ya mkutano wa EAC yalimtaka Rais Tshisekedi kuzungumza na kundi la waasi la M23 na makundi mengine ya waasi kwa lengo la kusimamisha mapigano.
Pia, maazimio ya Sadc kwa upande wake walimtaka Rais Kagame kuondoa majeshi yake DRC na kumtaka aache kuliunga mkono kundi la M23.
Ijue siri ya kufanyika Tanzania
Tanzania imekuwa mwenyeji wa mikutano mingi ya usuluhishi wa migogoro ya nchi jirani kama DRC, Burundi na Rwanda kutokana na historia yake ya amani na ushiriki wake katika kulinda amani bila tamaa ya kunufaika kisiasa au kijeshi.
Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia cha Salim Ahmed Salim, Denis Konga, amesema Tanzania imejijengea heshima kwa kusaidia kurejesha amani bila kutamani kubaki kwenye nchi nyingine.
“Jeshi letu lilikwenda Uganda wakati wa Vita vya Kagera na likairudisha nchi kwa wenyewe. Hali kadhalika, tumesaidia Comoro na DRC bila nia ya kung’ang’ania madaraka,” amesema.
Amesema uimara wa Serikali na mchakato wa mabadiliko ya uongozi Tanzania umeimarisha uaminifu wake katika jamii ya kimataifa.
Pia, ukaribu wake na DRC unalifanya taifa hili kuwa mstari wa mbele katika usuluhishi ili kuzuia wimbi la wakimbizi na athari za kiusalama.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesisitiza kuwa Tanzania siku zote imekuwa msitari wa mbele kusaidia majirani zake.
“Kama nyumba ya jirani inaungua, hatuwezi kuiacha iendelee kuungua, lazima tusogee kusaidia kuuzima moto huo,” amesema.
Brigedia Jenerali Mstaafu, Balozi Francis Mndolwa, amesema dhamira hii iliasisiwa na Mwalimu Nyerere, aliyehakikisha Tanzania inabaki kuwa nguzo ya amani barani Afrika.
Amesema kwa mantiki hiyo, viongozi waliomfuata, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, wameendelea kusimamia sera za amani na mshikamano wa kikanda.
Nyamwasa, Malema wamvaa Kagame
Wakati Rais wa Rwanda, Paul Kagame akisema kuwa hajui kama kuna majeshi ya nchi yake nchini DRC, aliyekuwa mkuu wa majeshi na idara ya usalama wa Rwanda, Jenerali Faustin Kayumba Nyamwasa amesema kauli ya Kagame ni hadaa.
Akizungumza na mtandao wa Extra Africa leo, Februari 4, 2025, Nyamwasa aliyewahi kuwa mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda na mkuu wa idara ya usalama kuanzia 1998 hadi 2002, amesema mara kadhaa Kagame amekiri kuwepo kwa majeshi ya Rwanda nchini DRC.
“Mara kwa mara nimemsikia Rais Paul Kagame kwenye televisheni akikiri kuwepo kwa majeshi ya Rwanda nchini DR Congo, anasema kama majeshi yapo huko kwa nini yasiwepo huko? Kwa hiyo hapo amekubali,” amesema.
Katika hatua nyingine, Kiongozi wa chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) cha Afrika Kusini, Julius Malema ameitaka Serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua kwa kauli za Rais Kagame kwa nchi hiyo.
Akizungumza kupitia mtandao wa Youtube, Malema amesema maneno anayotoa Rais Kagame hayamlengi tu Rais Ramaphosa, bali Waafrika Kusini wote.
“Unajua alipokuwa akimsema Rais alikuwa anatusema sisi, hawezi kutueleza sisi kama hivyo, hawezi kuua watu wetu kama hivyo,” amesema.