BEKI wa Tabora United, Salum Chuku atakuwa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu kuuguza majeraha ya goti aliyoyapata katika duru la kwanza la Ligi Kuu Bara wakati akiichezea timu hiyo dhidi ya maafande wa Tanzania Prisons.
Chuku ambaye amefanyiwa upasuaji wa goti amesema hali yake inaendelea vizuri na anaendelea na matibabu kwa matumaini ya kurejea uwanjani akiwa imara zaidi, ingawa amekiri haitakuwa kwa kiwango cha juu na inahitajika uvumilivu mkubwa.
“Si rahisi kukaa nje ya uwanja muda mrefu, hata hivyo, bado nina imani na matibabu yangu na wataalamu wanaonishughulikia,” alisema na kuongeza,
“Licha ya maumivu ya mwili, maumivu ya kiakili pia yalikuwa makali. Nilikumbwa na wasiwasi.”
Chuku anaamini nyota wenzake wa timu hiyo watapambana kuhakikisha inamaliza nafasi ya juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na hadi sasa baada ya mechi 16 imefikisha pointi 25 na iko nafasi ya tano.
“Kama ilivyo kwa kila mchezaji ambaye ana umoja na timu yake, mimi pia ninaendelea kuwa na matumaini na wachezaji wenzangu. Hata kama sitakuwa uwanjani, nafahamu tutapambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” amesema Chuku na kusisitiza mafanikio ya timu hiyo yanategemea mshikamamo na juhudi za kila mchezaji.
00000000000
Zidane, Landry wampa mzuka Taoussi
ELIYA SOLOMON
KOCHA wa Azam FC, Rachid Taoussi amevutiwa na viwango vya wachezaji wake wapya, Landry Zouzou na Zidane Sereri waliosajiliwa dirisha dogo la usajili lililopita kwa lengo la kuimarisha kikosi hicho.
Taoussi ameonyesha kuridhishwa na uwezo wa wachezaji hao kwani wameonyesha viwango vizuri mazoezini na anasubiri kuona watakachofanya kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho inakoshiriki timu hiyo.
Azam inatarajiwa kushuka Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Februari 6 dhidi ya KMC na Taoussi anatarajia nyota hao wapya watakuwa na mchango mkubwa kwenye mchezo huo.
“Tunafuraha nao, wamekuwa wakisaidiwa na wenzao kuhakikisha wanajisikia vizuri, ni wachezaji wazuri na tuna imani wataongeza kitu kwenye timu,” alisema kocha huyo.
Zouzou aliyesajiliwa kutoka AFAD Djékanou ya Ivory Coast, anatarajiwa kuchukua nafasi ya Yannick Bangala, aliyekuwa na mchango mkubwa katika eneo la beki alikokua akicheza sambamba na Mcolombia, Yeison Fuentes.
Hata hivyo, Zouzou anaonekana ataweza kufanya vizuri katika eneo hilo kutokana na nguvu na kasi aliyonayo, huku kocha akimwelezea ni mchezaji mwenye sifa zote za kuwa beki mzuri na ataziba vyema nafasi ya Bangala.
Kwa upande mwingine, Sereri aliyesajiliwa kutoka Dodoma Jiji, atakuwa na jukumu la kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Azam FC akisaidia na nyota wengine kama Gibril Sillah, Nassor Saadun na wengine.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, Azam inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 36 baada ya michezo 16 na inawania nafasi za juu ili ishiriki michuano ya kimataifa msimu ujao baada ya kuishia hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.