SAMIA: DUNIA IMETAMBUA JITIHADA ZA TANZANIA KATIKA SEKTA YA AFYA

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa Tuzo Maalum ya Kimataifa ya The Global Goalkeeper Award inathibitisha kuwa dunia imetambua juhudi za Tanzania katika kuboresha huduma za afya, hususan kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.

Rais Dkt. Samia amesema kuwa serikali anayoiongoza imeweka mipango madhubuti na kuongeza jitihada zaidi ili kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, Tanzania inavuka lengo la kimataifa la kupunguza vifo vya akina mama, watoto wachanga na watoto chini ya miaka mitano.

Mhe. Rais Dkt. Samia aliyasema hayo leo Jumanne, tarehe 4 Februari 2025, alipowahutubia waandishi wa habari mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Dodoma, akitokea jijini Dar es Salaam, ambako alipokea tuzo hiyo maalum ya kimataifa.

“Tuzo hii ina maana kubwa sana. Dunia imetambua jitihada zetu katika kuboresha huduma za afya, hasa afya ya mama na mtoto. Miaka minne iliyopita, vifo vya akina mama wakati wa kujifungua vilifikia 556 kwa kila vizazi hai 100,000.

“Lakini kwa sababu ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya—kujenga miundombinu, kununua vifaa tiba, kusomesha wataalamu na kuajiri wahudumu wa afya wa ngazi zote—tumeweza kupunguza vifo hivyo vya akina mama na watoto. Kwa akina mama, tumevishusha kutoka 556 hadi 104. Lengo la kimataifa kwa mwaka 2030 ni kufikia vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000. Kwa mwenendo huu, hakika tutafikia au hata kuvuka lengo hilo,” alisema Rais Dkt. Samia na kuongeza:

“Kwa watoto chini ya miaka mitano, tumepunguza vifo kwa kiwango kikubwa. Hata hivyo, bado tunakabiliana na changamoto kwa watoto wachanga, ambao wengi wao hupoteza maisha kutokana na sababu mbalimbali, zikiwemo matumizi ya dawa za kienyeji na kuchelewa kufika hospitalini. Vilevile, awali hatukuwa na vifaa vya kutosha kuokoa maisha yao, lakini sasa tumewekeza kwenye ununuzi wa vifaa hivyo, na kwa hakika hali itazidi kuimarika.”

Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa ingawa uongozi wake umechangia mafanikio haya, tuzo hiyo ni heshima kwa Watanzania wote, hususan watumishi wa sekta ya afya katika ngazi zote, ambao kwa juhudi zao wanawezesha huduma za afya bora kuwafikia wananchi.

Tuzo ya Global Goalkeeper Award, inayotolewa na Taasisi ya The Gates, hutunukiwa kwa viongozi wanaochangia kwa kiasi kikubwa katika kuharakisha maendeleo kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Rais Dkt. Samia amekuwa kiongozi wa kwanza barani Afrika kupokea tuzo hii, ikiwa ni uthibitisho wa mafanikio ya Tanzania katika mapambano dhidi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.






Related Posts