Simulizi ya mume wa mstaafu aliyekufa ajalini

Arusha: Mume wa mwalimu mstaafu aliyefariki dunia kwenye ajali ya gari amesimulia jinsi mkewe, Apaikunda Ayo (61), alivyojipanga kutumia fedha za mafao kununua gari la familia.

Simulizi hiyo imetolewa na mume wa marehemu, Exaud Mbise, wakati wa maziko yaliyofanyika leo, Jumanne, Februari 4, 2025, nyumbani kwa marehemu, Kijiji cha Imbaseni, wilayani Arumeru, Mkoa wa Arusha.

“Baada ya kumaliza kusomesha watoto wangu, nilikuwa sina gari; lile lilikuwa la familia, halikuwa la biashara. Lengo lilikuwa, tukitaka kwenda mahali, tuwe na usafiri wetu wenyewe. Mke wangu alistaafu mwaka jana, akawa amelipwa mafao yake.

“Tukakaa na kushauriana kwamba katika mafao, tulipanga vitu vingi. Mimi hela yangu na mke wangu ni zetu wote. Kati ya vitu tulivyopanga ni kununua lile gari, kisha mipango mingine,” amesema Mbise.

Mbise amesema yeye na mkewe (Ayo) waliagiza gari hilo nchini Japan kupitia mtoto wa dada yake, ila kulitokea changamoto kadhaa, ikiwemo mfumo wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), hivyo gari likachelewa kufika.

Amesema Jumatano ya wiki iliyopita walipata taarifa kuwa gari litatoka bandarini usiku, na Alhamisi walielezwa kila kitu kilikuwa kimekamilika.

“Tulikaa na mama, akasema mtoto amepata mtu anayekuja Arusha ambaye anafuata gari lingine, hivyo tumtumie kwani itakuwa rahisi yeye alete moja kwa mpaka Arusha. Mama akaenda Alhamisi.”

“Siku ya tukio, walianza safari. Tukawa tunawasiliana, na saa moja mwanangu aliyepo hapa nyumbani, wakamjulisha wako Njia Panda, hivyo watakaribia nyumbani wakati wowote,” amesema.

Amesema baada ya muda alipigiwa simu na Mark (kwa sasa marehemu), aliyemtaka ajiandae kwenda kuwapokea eneo la Momella.

“Saa mbili kasoro (asubuhi) nikapiga simu, nikajiandaa, na baada ya muda nikampigia mke wangu. Hakupokea. Kijana wangu hakupokea. Akapokea mtu mmoja, kumbe ni polisi. Akanieleza, ‘Wewe ni nani?’ Nikamjibu, ‘Huyu mwenye simu ni mke wangu.’

“Akaniuliza jina lake, nikamjibu. Akaniambia ameona kitambulisho, akaniuliza na kijana. Nikamjibu ni mtoto wangu, na mwingine wa tatu alikuwa ni dereva aliyeleta gari,” amesema.

Mbise amesema kuwa polisi huyo aliwajulisha kuwa hao watu wamepata ajali na wanapelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi. Wameumia, ila siyo sana.

“Nikatulia, na baada ya dakika tano nikampigia simu akaniambia nikueleze ukweli, ‘Hawa watu hapa tunawaingiza mortuary KCMC.’ Nikalazimika kujiandaa, nikaenda polisi, nikaenda hospitali kuthibitisha miili yote na jinsi gari lilivyo, kiukweli, halifai,” amesema Mbise.

Ayo (61), aliyekuwa mwalimu mstaafu wa Shule ya Msingi Imbaseni, mwanaye wa mwisho, Mark Exaud (22), na Paul Sita (25), aliyekuwa dereva wa gari hilo, walipata ajali baada ya gari lao aina ya Toyota RAV4 kugongana na basi la kampuni ya Esther Luxury.

Jana, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Imbaseni, Mwalimu Naetwe Emmanuel, akimzungumzia Ayo alisema wamepoteza mshauri katika utekelezaji wa majukumu yake.

Alisema kuwa amefanya kazi na Ayo kwa miaka miwili kabla hajastaafu Oktoba 2024, na kuwa wao kama ofisi walifanya sherehe ya kumuaga Desemba 6, 2024, na kwamba bado walikuwa wakiendelea kushirikiana naye katika masuala ya kijamii.

Related Posts