SHIRIKA la viwango Tanzania (TBS) limeendelea kutoa elimu kwa wazalishaji, waagizaji sambamba na wasambazaji wa bidhaa yenye lengo la kuhakikisha wanafuata matakwa ya Sheria za Viwango kwa kuingiza sokoni bidhaa zinazokidhi viwango.
Akizungumza na waandishi wa habari, January 30,2025 kwenye maadhiamisho ya wiki ya Sheria Kanda ya Dar es Salaam katika viwanja vya mnazi Mmoja,Afisa Masoko Mwandamizi TBS, Rhoda Mayugu amesema kuwa kupitia maadhimisho hayo wamelenga pia kuwakumbusha wazalishaji wa bidhaa kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa zinathibitishwa ubora wake na TBS.
Aidha Rhoda ameeleza kuwa itakuwa ni kosa ikibainika kuwa mzalishaji au msambazaji wa bidhaa ameingiza bidhaa ambazo hazijakidhi matakwa ya Sheria za Viwango.
Hata hivyo Rhoda amesema kuwa TBS inatoa huduma ya uthibitishaji bure kwa wajasiriamali wadogo na wakati ambao wanatakiwa kuanzia SIDO ambapo atapatiwa barua ya utambulisho itakayomsaidia anapofika katika ofisi zao.
Sambamba na hayo Rhoda amesisitiza waagizaji wa bidhaa nje ya nchi kufuata utaratibu ambapo TBS inatoa huduma ya kukagua bidhaa nje ya nchi ili kuepusha hasara.
“Kuepuka usumbufu na hasara zinazoweza kuepukika tunatoa wito kwa waagizaji wa bidhaa kuhakikisha bidhaa hizo zinapimwa kabla hazijaja hapa nchini”Amesema.