‘Uchawi’ wa Ramovic Yanga, upo hapa!

KOCHA wa Yanga Mjerumani Sead Ramovic ni wazi gari limemwakia baada ya kushinda michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu Bara, huku ikionekana akibebwa zaidi na nyota watatu, Clement Mzize, Prince Dube na Pacome Zouzoua kutokana na namba walizonazo hadi sasa ndani ya matokeo ya timu hiyo.

Ramovic aliyejiunga na Yanga, Novemba 15, mwaka jana akitokea TS Galaxy ya Afrika Kusini akichukua nafasi iliyoachwa na Miguel Gamondi ameiongoza Yanga kushinda michezo sita akifunga mabao 22 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara mbili, huku nyota hao watatu wakifunika katika uchangiaji mabao.

Katika mabao hayo 22, nyota watatu ndio waliofunga mengi wakiongozwa na Clement Mzize na Prince Dube ambao kila mmoja ana matano, huku Pacome Zouzoua akiwa na manne, ilihali Kennedy Musonda, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Mudathir Yahya wakifunga mawili.

Mwingine ni kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz KI aliyefunga moja, huku lingine kati ya hayo 22 ni la kujifunga kwa beki wa Fountain Gate, Jackson Shiga wakati kikosi hicho cha ‘Wana Jangwani’ kiliposhinda mabao 5-0, Desemba 29, mwaka jana.

Kati ya nyota hao watatu, Mzize ndiye anayeongoza kwa kuchangia mabao mengi akifanya hivyo mara nane, baada ya kufunga matano na kuasisti matatu, akifuatiwa na Pacome aliyechangia saba kwa kufunga manne na kuasisti matatu.

Kwa upande wa Dube pia amehusika katika mabao saba baada ya kufunga matano na kuasisti mawili, huku Mudathir Yahya akifuatia baada ya kutupia kambani mawili na kuasisti mawili, wakati Aziz Ki amefunga bao moja tu na kuasisti mbili.

Kiwango bora ambacho kinaendelea kuonyeshwa na nyota hao watatu, Mzize, Pacome na Dube, kinawafanya pia kujiweka katika mazingira mazuri ya kuvunja rekodi zao za mabao ya Ligi Kuu walizoziweka msimu uliopita, ikiwa tu wataendeleza moto huo.

Kwa Mzize tayari ameivuka rekodi yake ya msimu uliopita aliofunga mabao sita na sasa amefikisha saba, huku kwa upande wa Dube aliyeichezea matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC msimu uliopita akifunga saba na kwa sasa amefikisha matano.

Pacome anaweza pia kuivunja rekodi yake ya mabao ikiwa ataendeleza kiwango bora anachokionyesha na kikosi hicho na msimu uliopita alioandamwa na majeraha ya mara kwa mara alifunga mabao saba, ingawa hadi muda huu tayari amefunga sita.

Kiwango bora cha mastaa hao ambao wameifanya Yanga kuendelea kushika nafasi ya pili na pointi 42, nyuma ya wapinzani wao Simba wenye 43, kimetokana na tangu mara ya mwisho ilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Tabora United, Novemba 7, mwaka jana.

Baada ya mchezo wa Februari Mosi mwaka huu ambao Yanga ilishinda mabao 4-0, dhidi ya Kagera Sugar, Ramovic alinukuliwa akieleza furaha yake ni kuona maendeleo mazuri ya wachezaji ndani ya kikosi hicho, huku akiwataka kufunga mabao zaidi.

Yanga kesho Jumatano itaikaribisha KenGold inayoburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi sita tu baada ya mechi 16, huku zikiwa na matokeo ya mchezo wa kwanza uliopigwa jijini Mbeya kwa watetezi hao kushinda kwa mbinde kwa bao 1-0 lililowekwa kimiani kwa kichwa na Ibrahim Bacca.

Related Posts