Uchunguzi kesi ya Wapakistani wanaodaiwa kusafirisha dawa za kulevya waendelea

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeieleza Mahakama bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine na methamphetamine zenye uzito wa kilo 447.3 inayowakabili raia wanane wa Pakistani.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa hizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam (50) maarufu kama Tayeb, Immambakshi Kudhabakishi (55).

Wengine ni Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama hiyo leo Jumanne Februari 4, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

New Content Item (1)

Raia nane wa Pakistan wanaokabiliwa na mashtaka ya kusafirisha shehena ya dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphetamine zenye uzito wa kilo 447, wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne

Wakili Kasala amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mhini, kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wapo mbele ya Mahakama hiyo.

Wakili alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea hivyo, wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mhini amewaeleza washtakiwa hao kuwa,  hakimu anayesikiliza kesi yao Beda Nyaki ameanza likizo, hivyo kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 17, 2025 kwa kutajwa na wataendelea kuwa rumande washtakiwa hao.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, kesi hiyo inatafsiriwa na mkalimaniwa Salma Mohamed, raia wa Pakistani kila kinachoelezwa Mahakamani kutoka Kiingereza kwenda lugha ya Urdu inayotumika nchini Pakistani.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Januari 9, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025.

Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha kemikali ya kutengenezea dawa.

Wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 25, 2024 katika eneo la Navy lililopo Kigamboni wilaya ya Kigamboni, kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine.

Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kulevya aina heroine, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 25, 2024 eneo la Navy Kigamboni na  walikutwa na heroine zenye uzito wa kilo 22.53.

Related Posts