Upelelezi wakwamisha kesi ya mauaji kiongozi wa CCM

Iringa. Kesi ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani Kilolo, Christina Kibiki inayowakabili viongozi watano wa chama hicho imehairishwa kwa mara ya tatu sasa.

Kesi hiyo imeahirishwa leo Februari 4, 2025 baada ya upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Atupele Makoga kuomba ahirisho katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa ili kukamilisha upelelezi.

Makoga ameiomba Mahakama hiyo kutokana na upelelezi huo kutokamilika, kesi hiyo ihairishwe mpaka Februari 12, 2025.

Akijibu ombi hilo, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Adelina Ngwaya anayesikiliza kesi hiyo katika hatua ya awali, amesema kutokana na ratiba za Mahakama, Februari 12 hakutokuwa na nafasi hivyo kesi itasikilizwa tena Februari 17, 2025.

Kwa upande wa utetezi unaosimamiwa na mawakili Barnabas Nyalusi, Neema Chacha, Gloria Mwandelema na Clever Kapinga wameuomba upande wa Jamhuri kuongeza kasi kufanya upelelezi ili taratibu za kisheria zichukuliwe.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Diwani wa Nyanzwa, Boniface Ugwale, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Kilolo, Hedikosi Kimwaga, Katibu wa mbunge wa Kilolo, Kefa Walles, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mlandege, Wille Chikweo na Silla Kimwaga.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo la mauaji Novemba 12, 2024 nyumbani kwa Kibiki eneo la Banawanu, Kata ya Mseke mkoani Iringa.

Related Posts