VIDEO: Bunge laazimia Serikali isitegemee msaada fedha za Ukimwi

Dodoma. Bunge limeazimia Serikali itekeleze mpango wa kupata rasilimali za ndani kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi bila kutegemea msaada wa wafadhili.

Azimio hilo limefikiwa leo Februari 4, 2025, ikiwa ni siku chache baada ya Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kutangaza kusitisha utoaji fedha mpya na usambazaji wa fedha chini ya makubaliano ya malengo ya Maendeleo (DOAGs), hadi uhakiki kwa programu za msaada wa nchi zinazofadhiliwa na USAID utakapokamilika.

Wakati mchakato wa kuhakikisha msaada wa nje unalingana na ajenda ya sera ya nje ya Rais Donald Trump ukitarajiwa kutolewa ndani ya siku 30, uhakiki huo unatarajiwa kukamilika ndani ya siku 85 kuanzia Januari 24, 2025.

Azimio la Bunge limefikiwa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu kuwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa shughuli zake katika kipindi cha kati ya Februari 2024 hadi Februari 2025.

Kingu amesema kiwango kikubwa cha utekelezaji wa afua za VVU na Ukimwi nchini hutegemea fedha za wafadhili kutoka nje ya nchi.

“Ufadhili huo ukifikia ukomo unaweza kusababisha kwa kiasi kikubwa nchi kupunguza kasi ya kupambana na janga hilo kwa kukosa fedha za kutosha,” amesema.

Amependekeza Bunge liazimie kwamba Serikali itekeleze kikamilifu mpango wa uendelevu wa mwitikio wa VVU na Ukimwi nchini, ili kupata rasilimali endelevu za ndani katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi bila kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili.

Baada ya pendekezo hilo, Naibu Spika, Mussa Zungu aliwahoji wabunge nao wakapitisha azimio hilo kwa wingi wa sauti. “Ndiyoooo”.

Kabla ya kupitisha azimio hilo, mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Jacqueline Kainja alichangoa mjadala huo akisema Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS) inategemea kwa kiasi kikubwa fedha za wafadhili wa nje ya nchi, hususan kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani (PEPFAR) na Mfuko wa Dunia wa Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu ili kutekeleza afua hizo.

“Bajeti ya 2024/2025, katika Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) asilimia 86 ni fedha kutoka nje ya nchi ambazo ni sawa na Sh11.36 bilioni ukilinganisha na fedha za ndani ambazo ni sawa na asilimia 14 yaani Sh1.8 bilioni,” amesema.

“Tukiangalia hivi sasa wenzetu Marekani Rais ametangaza kuwa anasitisha huduma katika mfuko wake huo wa dharura, hatujajua kuwa mfuko ule utasimamishwa kwa muda gani, kama Taifa tunajipangaje?” amehoji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu akiwasilisha taarifa ya mwaka 2024-2025 ya kamati hiyo leo Februari 4, 2025 bungeni jijini Dodoma. Picha na Hamis Mniha

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imesema PEPFAR umejumuishwa katika msamaha wa misaada ya kibinadamu ya kuokoa maisha wakati wa kusitishwa msaada wa kigeni kwa siku 90.

Miongoni mwa shughuli zilizoruhusiwa ni utunzaji wa watu wenye VVU kwa lengo la kuokoa maisha, upimaji na ushauri, kuzuia na matibabu ya maambukizi ya kifua kikuu, huduma za maabara, ununuzi na usambazaji wa bidhaa za afya na dawa.

PEPFAR pia imeruhusiwa kutoa huduma za kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto.

Saa chache baada ya kuingia madarakani Januari 20, 2025 Rais Donald Trump aliamuru kusitishwa kwa misaada ya kigeni ili kuchunguzwa iwapo inalingana na sera yake ya kigeni ya “Marekani Kwanza.”

Kainja ameiomba Serikali mpango wa uendelevu wa mwitikio wa VVU na Ukimwi uliozinduliwa Desemba mosi, 2024 uendelee kusimamiwa na kufanya kazi ili kuondoa sintofahamu kwa wananchi ambao wanaishi na VVU.

Mbali na suala hilo, Kingu amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 imebainishwa vyanzo vya fedha za kugharamia watu wasio na uwezo kupitia Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote (UHC), ambavyo vilitarajiwa kukusanya Sh173.5 bilioni, lakini kiasi kilichokusanya ni kidogo.

Amesema hadi Novemba 23, 2024, kiwango kilichokusanywa ni Sh47.13 bilioni pekee sawa na asilimia 27.

Amesema kwa kuwa jitihada kadhaa zimefanyika ikiwa ni pamoja na kubainisha vyanzo vya fedha za mfuko huo, kamati inapendekeza kwa Bunge liazimie kwamba, Serikali iwashirikishe wadau kutoka sekta binafsi kuchangia fedha za mfuko wa kugharimia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo, suala ambalo pia liliazimiwa na Bunge.

Kuhusu changamoto za uendeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kamati imependekeza kufanyika marekebisho kwa Sheria ya mfuko huo sura namba 395 ili kuziondoa.

Kingu amesema changamoto hizo husababisha athari hasi katika uendeshaji, hivyo marekebisho yalenge kuitambua sekta binafsi ya afya ambayo ni mdau muhimu.

“Iimarishe mifumo ya Tehama ili kulipa watoa huduma za afya kwa wakati na kudhibiti udanganyifu wa matumizi ya bima ya afya, kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa huduma ya bima ya afya na mtindo bora wa maisha kwa lengo la kukabiliana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza,” amesema.

Kuhusu udhibiti wa Ukimwi, magonjwa ya ngono na homa kamati imelitaka Bunge liazimie Serikali iweke mikakati ya kutenga fedha za ndani kwa ajili ya mapambano ya magonjwa ya ngono na homa ya ini na iongeze kasi ya utoaji wa elimu kuhusu maambukizi ya magonjwa hayo, suala ambalo pia lilipitishwa.

Kingu amesema kamati inapendekeza Serikali ikamilishe mchakato wa kuandaa sheria ya uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa chembechembe na viungo vya mwili wa binadamu ili kuweka namna nzuri ya utoaji wa huduma hiyo kwa kulinda haki za binadamu, kuhakikisha usalama wa afya kwa wananchi na kuzuia biashara haramu ya viungo vya mwili wa binadamu.

“Kufanyika kwa huduma hizo bila uwepo wa sheria rasmi, kunaweza kusababisha athari hasi kwa jamii ikiwa ni pamoja na kukiukwa kwa haki za binadamu na kuibuka kwa biashara haramu ya viungo vya binadamu,” amesema.

Katika hatua nyingine, wabunge wameazimia Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kurejesha fedha za michango zilizolipwa na wastaafu badala ya waajiri.

Azimio hilo limefikiwa baada ya kubainika baadhi ya wastaafu wamelazimika kulipa madeni ya michango wanayodaiwa waajiri wao ili kulipwa mafao kinyume cha Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma Sura 371.

Akiwasilisha bungeni taarifa ya mwaka ya Kamati ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Fatuma Toufiq, amesema PSSSF inapaswa kurejesha na kuzidai fedha hizo kwa waajiri kama sheria inavyoelekeza.

“Kitendo hiki kinaondoa imani ya mwajiriwa kwa mfuko huo, hakipaswi kuvumiliwa na Bunge ambalo ndilo lenye mamlaka ya utungaji wa sheria, kinakinzana na lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa kuhakikisha ustawi wa wanachama,” amesema.

Ametaja azimio jingine ni mifuko iache mara moja utaratibu wa kutoa namba za malipo kwa wastaafu ili walipe michango ambayo haijawasilishwa na mwajiri wakati wakifuatilia mafao yao.

Pia, mifuko ichukue hatua kali za kisheria kwa waajiri wasiowasilisha michango kwa mujibu wa sheria.

“Wastaafu hawa wanalazimika kulipa kwa kuwa hawana kingine wanachotegemea zaidi ya mafao yao. Suala hili si sawa hata kidogo, hasa ikizingatiwa kuwa sheria haizuii mstaafu kulipwa mafao yake hata kama mwajiri hajakamilisha michango yake,” amesema.

Amesema PSSSF inawawajibisha wastaafu kwa makosa yake ya kushindwa kusimamia sheria kwa kuhakikisha mwajiri anawasilisha michango kwa wakati.

Toufiq amesema Serikali ichukue hatua za haraka na madhubuti, ikiwa ni pamoja na kuyafuta mashirika ambayo yanajihusisha na masuala ya mmomonyoko wa maadili kinyume cha tamaduni za nchi, yanayojihusisha na utakatishaji fedha na mashirika yanayojihusisha na siasa wakati wa uchaguzi.

Mbali na hayo, amesema Sh937.3 milioni za Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) zilizokopeshwa hazijarejeshwa hali inayoathiri utolewaji wa mikopo kwa wanawake na tija iliyokusudiwa.

Wakichangia taarifa hiyo, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ali Khamis na Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema Serikali itafanyia kazi hoja na maazimio yote yaliyotolewa na Bunge.

Related Posts