Hatimaye Serikali imezindua Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la 2023 jijini Dodoma hivi karibuni.
Uzinduzi huo unafuatia kukamilika kwa nchakato wa mapitio ya sera hiyo iliyozinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014.
Akizindua sera hiyo mbele ya wadau mbalimbali wa elimu nchini, Rais Samia Suluhu Hassan alitaja mambo kadhaa yaliyoisukuma Serikali yake kuifanyia mapitio sera hiyo punde tu baada ya kuingia madarakani.
Alizitaja sababu hizo ni ni kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia itakayosababisha baadhi ya kada nyingine kukua na nyingine kutoweka.
Sababu ya pili ni utandawazi ambao unatoa fursa ya bidhaa na huduma kutoka sehemu moja ya dunia kwenda nyingine kwa njia rahisi na bila kulazimika kuwa na msimamizi.
Pia, ongezeko la idadi ya watu lisiloendana na kasi ya ukuaji wa uchumi ni sababu nyingine iliyomsukuma Rais Samia kutaka mapitio hayo ya sera na mitaalaa.
“Ukuaji wa asilimia 3.2 kwa mwaka inakadiriwa kwamba ifikapo mwaka 2044 idadi ya watu hapa nchini itakuwa milioni 123 na hivyo kuongeza uhitaji wa kazi na ajira kwa vijana, hivyo ninachokiona huko mbele kinatufanya tuwe na maandalizi ya kutosha kwa kuinua ubora wa elimu yetu,’’ alisema.
Aliongeza: Kwa kutoa elimu bora zaidi ya kisasa na kuandaa vizuri zaidi vijana wetu ili waweze kumudu stadi muhimu zitakazowawezesha kuajiriwa au kujiajiri. Elimu itakayowafanya vijana wetu waweze kushindana kikanda na kimataifa, kuwajengea ujasiri kuweza kujiamini. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunaandaa mazingira mazuri ya upepo kuwapepea vijana wetu badala ya kuwapeperusha.’’
Kwa mujibu wa Serikali, maono ya sera hiyo ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika, mwenye maarifa, stadi na mtazamo chanya utakaomwezesha kuchangia katika kuleta maendeleo endelevu ya Taifa.
Kuhusu dhima, sera inalenga kuinua ubora wa elimu na mafunzo kwa kuweka mifumo na taratibu zitakazowezesha kupata idadi kubwa ya Watanzania walioelimika, wenye stadi na wanaopenda kujiendeleza kielimu ili waweze kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.
Kufuatia uzinduzi huo, Mwananchi liliwatafuta baadhi ya wadau wa elimu waliotoa maoni ya namna sera hiyo inavyoweza kuwa na manufaa kwa Taifa.
Katibu wa Chama cha Walimu wa Shule Binafsi Nchini (TPTU) Julius Mabula anasema sera na hata mitalaa iliyoanzishwa kutokana na sera hiyo, ni jambi zuri ila tatizo analoliona ni uwezekano wa utekelezaji wake kuingiliwa na alichokiita siasa.
“Mitalaa ikisimamiwa kama ilivyo kwa sera yenyewe, ni mitaala ambayo baada ya miaka mitano ama 10 huko mbele, inaenda kuwa mkombozi kwa nchi yetu na tutakuwa na wasomi ambao ni mahiri na wataweza kujiajiri na kuajirika,”anasema na kufafanua kuwa anaposema siasa ni kama vile kutekeleza mtalaa huo pasipo kuwatazama walimu na kutatua changamoto zao.
Anasema hakuna mageuzi makubwa ya elimu yanayoweza kufaanikiwa, ikiwa walimu wataachwa kuelea katika dimbwi kubwa la changamoto.
“Tukitekeleza bila uwekezaji kwa walimu, hakutokuwa na manufaa. Kwanza tuwape mafunzo walimu ambao ni watekelezaji wa mtalaa huo. Kwa sababu nchi inahama kwenye mfumo mmoja na kwenda katika mfumo mwingine wa elimu, mafunzo kwa watekelezaji ni muhimu,”anaeleza.
Anasema wakati hilo likifanyiwa kazi, walimu hao wasiwe wale walio kwenye utumishi wa umma. Uhusishe pia walimu wa sekta binafsi anaosema idadi yao ni zaidi ya 150,000.
Anasema walimu wa sekta binafsi wamekuwa wakitengwa, japo na wao wanafanya kazi moja ya kumuelimisha mtoto wa Kitanzania.
Hata hivyo, alipokuwa akizindua sera hiyo, Rais Samia alisema Rais Samia amesema miongoni mwa mambo muhimu yatakayoangaliwa ili kufanikisha utekelezaji wa sera na mitalaa hiyo ni mapitio ya maslahi ya kada ya ualimu nchini.
Hatua hiyo inalenga kuipa hadhi inayostahili kada hiyo ambayo ndio mama wa taaluma zote akieleza kuwa mwalimu ndiyo kiungo wa utekelezaji wa sera na mitaala.
“Kwa maoni yangu ndio kiongozi wa elimu, hivyo katika maboresho haya lazima mwalimu awe katikati ya mduara wa maboresho yaliyofanyika na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki ili waendane na muelekeo wa sera hii,” alisema na kuongeza:
“Aidha, tutapitia upya maslahi ya kada ya walimu nchini ili kuipa hadhi inayostahili kama mama wa taaluma zote duniani.’’
Mdau mwingine wa elimu, Ochola Wayoga anasema utekelezaji wa sera hauwezi kufanikiwa kwa uwekezaji uliopo sasa.
“Nimeona Rais akifikiria kuhusu maslahi ya walimu, inawezekana ikawapa motisha. Kwa uwekezaji uliopo na mahitaji katika elimu sidhani kama tumefanya vya kutosha. Huwezi kuniambia mtoto awe na umahiri wakati hata choo hana shuleni,”anasema.
Wayoga anashauri kuwe na uwekezaji unaoendana na matarajio ya sera, kwa kuwa sera sio karatasi ya kuzinduliwa bali ni mpango endelevu.
Anasema uwekezaji mdogo ndio uliofanya kushindwa kutekelezeka kwa sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, kwa kuwa hakukuwa na madarasa ya kutosha wala vitabu vya kufundishia.
“Sera ilipita bila kuangalia gharama zikoje, sasa huwezi kupitisha sera bila kuangalia gharama zikoje, sasa ile ilikuwa ni siasa tupu. Lakini nchi ilikuwa haijajiandaa kupokea wanafunzi wengi kwa wakati mmoja,”anasema.
Hata hivyo, anasema alichofurahia katika sera mpya ni utunzi wa vitabu vya darasa la tatu na la nne, anavyoeleza kuwa ni vigumu, hivyo mtoto akivisoma anaweza kujijengea umahiri wa kutosha.
Mwalimu Yasinta Damiani kutoka Shule ya Trust ST Patrick ya jijini Arusha, anasema sera hiyo imekuja wakati mwafaka, kwani kuna mlundikano wa vijana mtaani ambao hawana ajira wala hawawezi kujiajiri.
“Sera hii sasa inajibu changamoto ya ajira na itasaidia pia kupunguza uhalifu kwa kuwa vijana wengi watajikita katika kujiajiri badala ya kurundikana mitaani,”anasema.
Yasinta anasema jambo muhimu ni watekelezaji kuhakikisha miundombinu, vifaa na walimu kwa ajili ya utekelezaji vinakuwepo kwa kiwango cha kutosha.