Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia wanafunzi wawili wa kike wanaoishi vijibweni Kigamboni, wakituhumiwa kujiteka wenyewe huku wakiwataka wazazi wao kuwatumia fedha kwa njia ya simu wakidai wasipotuma wangepotezwa.
Kamanda wa polisi kanda hiyo, Jumanne Murilo amesema hayo leo Jumanne, Januari 4, 2025 na kuongeza kuwa, wanafunzi hao ni wa sekondari wa kidato cha pili (16) na mwanafunzi wa shule ya msingi darasa la saba (12), waliokutwa eneo la Longoni Beach Kigamboni.
Murilo amesema wanafunzi hao walitoweka Januari 26, 2025 nyumbani kwao na kuelekea eneo la Longoni Beach kufanya starehe na Januari 27, 2025 asubuhi walielekea Tungi hadi walipokamatwa.
Amesema Jeshi la Polisi lilifuatilia na kubaini watoto hao walipokuwa na baada ya mahojiano walikiri kutengeneza tukio hilo la uongo ili wajipatie fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa wazazi wao baada ya kutoweka.
“Hawa watoto walikwenda kwenye starehe walikuwa wanahofia kurudi nyumbani walichofanya wakawapigia simu wazazi wao wakijifanya wametekwa huku wakidai watumiwe hela ili waachiwe,” amesema.
“Jeshi la Polisi tunaendelea na uchunguzi na tunashirikiana na mamlaka zingine ili kuhakikisha zinatoa hati za kisheria watuhumiwa wapelekwe mahakamani,” amesema Murilo.
Amesema watoto hao ni ndugu wanakaa nyumba moja walihojiwa na kuachiwa kwa dhamana.