Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amesema Serikali imechukua hatua madhubuti kudhibiti mianya ya ukwepaji kodi unaosababishwa na mabadiliko ya majina ya kampuni za kigeni kwa kuhakikisha Namba ya Utambulisho wa Kodi (TIN) inabaki ile ile hata kama kampuni itabadilisha jina.
Hayo ameyasema bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe. Michael Mwita Kembaki, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wawekezaji wa nje ambao kila baada ya miaka kadhaa hubadili majina ya Kampuni kwa lengo la kukwepa kodi.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa Sheria ya Kampuni, Sura 212, ambayo inawataka wawekezaji kutoa taarifa kwa Msajili wa Kampuni (BRELA) wanapobadilisha jina la kampuni.
“Historia ya mabadiliko yote ya majina ya kampuni huhifadhiwa kwenye kumbukumbu rasmi ili kuhakikisha majina mapya hayawezi kutumika kuficha madeni ya kodi au kushiriki katika shughuli zisizo halali”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa kupitia Sheria ya Usimamizi wa Kodi, Sura 438, Serikali pia imeweka sharti kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha Namba ya Utambulisho wa Kodi (TIN) inabaki ile ile hata kama kampuni itabadilisha jina kwa kuwa TIN hutumika kufuatilia historia ya ulipaji kodi wa kampuni, hivyo mabadiliko ya jina hayaondoi wala kufuta wajibu wa kodi.
Aidha, akieleza kuhusu kodi zinazotozwa wakati wa kubadili jina la Kampuni kwa watanzania na wageni, Dkt. Nchemba alisema kuwa kubadili jina la Kampuni haiathiri wala haihusiani na masuala ya kikodi.
Alisema kuwa kinachosababisha kuwepo na kodi au ukwepaji wa kodi ni mabadiliko ya umiliki kwa kuuza Hisa ambazo zitaleta kipato cha ziada ambacho kinatakiwa kulipiwa kodi kutokana na faida iliyopatikana.
“Kama mmiliki ni yuleyule ameamua kubadilisha jina la Kampuni kwa ajili ya matangazo ya kibiashara na Namba ya Mlipa Kodi ni ileile, haileti badiliko lolote kwenye kodi”, alifafanua Dkt. Nchemba.
Alisema kuna kampuni za nje ambazo zinamiliki sehemu ya kampuni nchini na hazina shughuli zaidi ya zinazofanyika Tanzania, ikitokea wamebadilishana umiliki unaozidi asilimia 50, hapo kuna kodi ambayo ni lazima ikusanywe.
Alisema Serikali imefanyia kazi kwa kiasi kikubwa suala hilo lililokuwa likijitokeza katika maeneo ya mawasiliano, madini na mengine na amewatoa hofu wabunge kuwa Serikali imeweka kwenye Sheria na inafuatilia kwa umakini panapotokea jambo hilo na kodi stahiki ya Serikali inakusanywa.
Waziri wa Fedha, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akijibu swali bungeni jijini Dodoma la Mbunge wa Tarime Mjini, Mhe. Michael Mwita Kembaki, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wawekezaji wa nje ambao kila baada ya miaka kadhaa hubadili majina ya Kampuni kwa lengo la kukwepa kodi.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)