Dar es Salaam. Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani umesema Serikali ina taarifa rasmi ya watu 24 wanaoaminika kuwa Watanzania wanaoshikiliwa na Mamlaka ya Uhamiaji na Forodha ya Marekani (ICE) kwa kuishi nchini humo kinyume cha sheria.
“ICE imetuarifu kwamba, watu wanne kati ya hao wameshakamilisha taratibu zote za kimahakama za kuondoshwa nchini Marekani, hivyo watarejeshwa Tanzania muda wowote kuanzia sasa. Watu 20 waliobaki wapo kwenye hatua mbalimbali za kesi zao za uhamiaji huko Marekani,” umeeleza ubalozi huo.
Ubalozi huo katika majibu ya maswali yaliyoulizwa na Mwananchi kuhusu Watanzania waishio Marekani kinyume cha sheria umesema:
“Bado hatujaelezwa ni lini Watanzania hao watarejeshwa nyumbani lakini tayari ubalozi wetu nchini Marekani umeombwa na mamlaka husika za nchi hiyo, nyaraka za kusafiria za Watanzania wawili kati ya wanne ambao wameshapewa amri ya kuondoshwa nchini Marekani. Hivyo, tunatarajia watasafirishwa wakati wowote kurejeshwa nyumbani.”
Hatua ya kuwarejesha Watanzania hao imetokana na mkakati wa Rais wa Marekani, Donald Trump wa kutaka watu wote wanaoishi nchini humo bila vibali kuondolewa mara moja.
Hivi karibuni, taarifa ya ICE ilisema hadi Novemba 24, 2024, wahamiaji 1,445,549 kutoka mataifa mbalimbali waliorodheshwa kwa ajili ya kurejeshwa makwao.
Idadi hiyo ni ya watu kutoka mataifa mbalimbali wanaoishi Marekani bila vibali.
Katika orodha ya ICE, kwa nchi za Afrika Mashariki, Kenya imetajwa kuwa na wahamiaji wengi wapatao 1,282, ikifuatiwa na Burundi (462), Uganda (393), Rwanda (338) na Tanzania ikiwa na watu 301.
Katika majibu ya ubalozi huo kwa Mwananchi leo Februari 4, 2025 kwa maswali yaliyowasilishwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, umesema Watanzania watakaorejeshwa nyumbani kutoka Marekani wataruhusiwa kusafiri kwenda nchi nyingine bila kizuizi chochote, lakini kwa upande wa Marekani, kwa sheria zilizopo sasa, wanaweza kuomba viza na kuruhusiwa kuingia nchini humo baada ya miaka 10.
Kwa mujibu wa ubalozi huo, Watanzania wanaorejeshwa nchini baada ya kuishi Marekani kinyume cha sheria watakapofika nyumbani watapokewa na Idara ya Uhamiaji.
Umesema taratibu za kiuhamiaji zitakapokamilika watakuwa huru kuendelea na maisha yao kama raia wengine wa Tanzania.
“Kwenye suala hili la Watanzania waliokamatwa kwa kuishi kinyume cha sheria nchini Marekani, Ubalozi wetu nchini humo unashirikiana na mamlaka husika za uhamiaji nchini Marekani kuthibitisha uraia wa waliowekwa vizuizini na mamlaka hizo na kutoa nyaraka za kusafiria wanapothibitisha kuwa watu hao ni raia wa Tanzania. Ikumbukwe kwamba, kuishi nchi yoyote bila vibali maalumu ni kosa la kisheria,” umesema ubalozi huo.
Mkurugenzi wa Diaspora Tanzania, Kelvin Nyamori akizungumza na Mwananchi leo Februari 4, 2025 amesema itakuwa changamoto kwa watu wanaorudishwa kama walidanganya mataifa yao ili wapate haki ya ukimbizi.
“Kuna sheria za uhamiaji za kila nchini na hawa waliondoka kwa utaratibu, ukitokea Tanzania huwezi kusingizia vita au ukimbizi, kwa kuwa Tanzania hatuna matukio hayo, wapo wengine wanajitafutia nchi ili apewe nyaraka.
“Matokeo yake ikitokea tatizo kama hili wanasakwa waliingiaje na hakuna nchi ina usalama wa juu kama Marekani, sasa kama uliingia ukiitwa Judy ukiwa Mtanzania na pasipoti yako inaonyesha tangu umeondoka hujawahi kurudi halafu sasa ni Kuruthumu wa Somalia, hii itakuwa changamoto nyingine,” amesema.
Ameshauri watu kufuata taratibu na kuwa na vibali wanapotoka nje ya nchi.