Kagame hajui kama kuna wanajeshi wa Rwanda nchini DRC

Kigali. Rais wa Rwanda, Paul Kagame amesema kuwa hafahamu kama majeshi yake yako Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mashariki mwa DRC ni eneo ambalo mapambano kati ya vikosi vya Jeshi la DRC (FARDC) na waasi wa Kundi la M23 yameshika kasi huku waasi hao wakidai kuushikilia Mji wa Goma nchini humo.

Mapigano kati ya pande hizo yanatajwa kusababisha vifo vya watu zaidi ya 700 huku zaidi ya 2,300 wakijeruhiwa

Jumuiya ya kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa (UN) imekuwa ikiishutumu Rwanda kwa kuwafadhili waasi hao wa M23, tuhuma ambazo Kagame amekuwa akizikanusha.

Kwa mujibu wa UN, inakadiriwa wanajeshi kati ya 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanasimamia na kuwasaidia wapiganaji wa M23 Mashariki mwa DRC kupambana na vikosi vya Serikali.

Katika mahojiano na CNN, Jumatatu Januari 3,2025, Kagame alipoulizwa iwapo kuna vikosi vyovyote vya Rwanda nchini DRC amejibu:

“Sifahamu,” amesema Kagame, pamoja na kuwa yeye (Kagame) ni Amiri Jeshi Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Rwanda

“Kuna vitu vingi ambavyo sivifahamu. Ila ukiniuliza kama kuna tatizo nchini Congo ambalo Rwanda inahusishwa na Rwanda itafanya kila iwezalo kujilinda nitakujibu asilimia 100,” amesema.

Msimamo wa Kagame, unakinzana na kauli ya M23 ambao Msemaji wao, Victor Tesongo aliieleza CNN kuwa kundi hilo linapokea ufadhiri kutoka Rwanda.

Tesongo amedai kuwa Rwanda ndiyo taifa ambalo linajali na kufuatilia mwenendo wa shughuli zao nchini DRC hususan wanapokabiliana na FARDC.

Waziri wa Mawasiliano wa DRC, Patrick Muyaya, aliieleza CNN Jumatatu iliyopita kuwa uwepo wa vikosi vya Rwanda nchini DRC unafahamika huku akisisitiza kuwa Kagame anapambana kufanya kila awezalo kukanusha ukweli huo.

“Katika kipindi cha siku 10 zilizopita, wataalamu kutoka UN, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu wa UN, Rais João Lourenço (wa Angola), na SADC wamethibitisha uwepo wa vikosi vya Rwanda nchini DRC. Ni Kagame pekee anayekanusha hilo,” amesema Muyaya.

Alipoulizwa na Mwandishi wa CNN, Larry Madowo kuwa mbinu anayoitumua inafanana na inayotumiwa na Rais Vladimir Putin nchini Russia kuwafadhiri vikosi vya kijeshi vinavyopingana na utawala wa Zelenskyy na hivyo kuivamia Ukraine amesema:

“Natambua kutakuwa na maneno mengi yanayozungumzwa.” alisema Kagame huku akisisitiza kuwa hawezi kumzuia mtu kuzungumza chochote anachojisikia.

“Ninaweza kuitwa chochote hata nikiitwa majina ya hovyo sina cha kufanya. Tutafanya kila tunachopaswa kufanya na tuhakikishe tunaishinda mitihani tunayopitia,” amesema.

Kagame alienda mbali na kuliita kundi la Democratic Forces for the Liberation of Rwanda (FDLR), kuwa linaendesha shughuli za kigaidi likiwa ndani ya DRC, jambo linalotishia usalama wa Rwanda.

Pia, aliishutumu Serikali ya DRC kuwa inahusika kuwafadhiri waasi hao wa FDLR kufanya shughuli za uasi dhidi ya Serikali ya Rwanda.

Rais huyo alisisitiza kuwa Rwanda itafanya kila iwezalo kujilinda dhidi ya uvamizi wa aina yoyote bila kutoa taarifa kuwa itajilinda kwa mbinu gani.

“Hakuna mtu hata iwe kutoka Umoja wa Mataifa atakayesaidia kuilinda mipaka yetu,” alisema Kagame.

Alipoulizwa tena iwapo ametuma Jeshi lake nchini DRC, Kagame alisema Rwanda itafanya kila iwezalo kujilinda dhidi ya uvamizi wa nje huku akimtaka mwandishi wa CNN kutafsiri kwa kadri atakavyoyaelewa maneno yake.

Kuwa mujibu wa Msemaji wa Serikali ya Rwanda alipozungumza na CNN alisema hadi kufikia jana (Jumatatu) raia wanne wa Rwanda walikuwa wameshauawa kutokana na mapigano kati ya M23, na vikosi vya Serikali ya DRC.

Wiki iliyoisha Rais Felix Tshisekedi wa DRC alitoa ahadi ya kujibu mapigo na kusema Serikali yake haitokuwa tayari kudhalilika wala kufedheheshwa na wapiganaji wa M23.

“Kiufanisi mapambano yetu hayatoishia Goma, lengo ni kwenda hadi kumng’oa Tshisekedi madarakani na kutafuta mwarobaini wa changamoto za raia wa alisema msemaji wa kundi hilo, Tesongo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.

Related Posts