MASHABIKI wa Simba wanatamba mitaani namna timu yao inavyopasua mawimbi kuutafuta ubingwa wa Ligi Kuu Bara, lakini ndani ya furaha hiyo kuna rekodi moja ya maana anaifukuzia kocha Fadlu Davids akiwazidi wazungu sita na mzawa mmoja.
Kabla ya Fadlu kutua Simba msimu huu, klabu hiyo imewahi kufundishwa na makocha tofauti akiwamo, Mualgeria Abdelhak Benchikha, Mbrazil Roberto Oliveira ‘Robertinho’, Mserbia Zoran Maki, Mhispania Pablo Franco, Mfaransa Didier Gomes, Wabelgiji Sven Vandenbroeck na Patrick Aussems.
Kama ulikuwa umesahau, Aussems aliyeifundisha Simba kati ya Julai 2018-Novemba 2019 ndiye aliyekuwa kocha wa mwisho kuiongoza Simba kushinda michezo 10 aliposhinda mechi 11 mfululizo kabla ya rekodi hiyo kusitishwa Aprili 19, 2019 ugenini dhidi ya Kagera Sugar alipolala kwa mabao 2-1.
Baada ya hapo hakuna kocha aliyefikisha hata mechi 10, lakini Fadlu wikiendi iliyopita alipowapiga Tabora United kwao mabao 3-0 akaifikisha mchezo wa 10 bila kupoteza akishinda mechi hizo za ligi mfululizo.
Fadlu amebakiza mchezo mmoja tu kuipiku rekodi hiyo ya Aussems hasa kama ataichapa Fountaion Gate kwenye mchezo wa ugenini wiki hii, mjini Babati mkoani Manyara.
Simba chini ya Fadlu imepoteza mechi moja tu dhidi ya Yanga ilikuwa Oktoba 19, 2024 ilipolala nyumbani kwa bao 1-0 na baada ya hapo kipigo hicho kilikuwa kama kimewaamsha wekundu hao ikitembeza vipigo kwa kila mpinzani iliyekutana naye uwanjani kwenye ligi.
Akizungumzia rekodi hiyo, Fadlu alisema kuimarika kwa kikosi chake kwa kila mchezaji kushindana kiukweli kuipigania timu yake ndiyo msingi wa muendelezo wa ubora wao uwanjani.
Fadlu alisema kwa sasa ana furaha kubwa kwa namna kikosi chake kinavyocheza kwenye ubora ambao wanautaka kwa kushinda mechi zao, pia wakiwa na ugumu kuruhusu mabao.
“Tumekuwa na mwendelezo mzuri, hivi ndiyo namna ambavyo timu yangu nataka icheze, tunatumia nafasi uwanjani lakini pia tuna uimara kwenye ulinzi,” alisema Fadlu na kuongeza.
“Nawapongeza sana wachezaji wangu kwa namna wanavyojituma kuanzia kwenye maandalizi yetu mpaka kwenye mechi zetu, tukiendelea kuweka hai hesabu zetu kutafuta malengo ambayo tumejiwekea.
“Kama unavyoona hakuna mechi rahisi, ukiwa unajiandaa unaona namna kila mpinzani anavyojipanga kuhakikisha tunazuiwa lakini mpira wetu na ubora wetu unaamua matokeo.”