Mifuko ya hifadhi ya jamii kulipa riba ucheleweshaji wa mafao

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeanzisha riba kwa mifuko ya hifadhi ya jamii itakayosababisha ucheweshaji wa mafao kwa wanachama huku Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ukilipa asilimia 15 wakati Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) utalipa asilimia tano.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Februari 4, 2025 na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alipokuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa viti maalumu (CCM), Fakharia Shomar Khamis.

Katika swali la msingi, Fakharia amehoji iwapo mstaafu aliyecheleweshewa kupata mafao anaweza kudai fedha kutokana na usumbufu alioupata wakati anasubiri mafao yake.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema Sheria za NSSF na PSSSF katika vifungu 49(3) na 43(3) mtawalia, vinaeleza endapo mfuko utachelewesha kulipa mafao kwa mwanachama na uchelewesho huo haukusababishwa na mwanachama mwenyewe au mwajiri, utalipa riba.

Mfuko utamlipa mwanachama huyo mafao yake pamoja na riba ya asilimia 15 kwa mwaka, kiasi atakachokuwa amelipwa kama mafao kwa Mfuko wa NSSF na asilimia tano  kwa Mfuko wa PSSSF.

Amesema sheria imetoa haki ya mwanachama kulipwa fidia endapo atacheleweshewa kulipwa mafao yake ikiwa ucheleweshaji huo umesababishwa na mfuko.

Katika maswali ya nyongeza, Fakharia amehoji ni sababu gani za msingi ambacho kinasababisha mafao kuchelewa.

Pia, amesema kwa kawaida Serikali inafahamu kustaafu kwa watumishi wao.

Amehoji wanaohusika na mafao ya wastaafu wanawadhibiti vipi ili wawajibike kwa sababu wao ni sehemu ya kufanya mafao ya wastaafu kuchelewa.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema moja ya changamoto iliyokuwepo awali ni wastaafu kuombwa nyaraka mbalimbali ikiwamo barua za kuajiriwa ambazo kimsingi zilitakiwa mwajiri kuwa nazo.

“Kulikuwa na changamoto ya ukinzani wa taarifa lakini baada ya kubaini changamoto hizo na nyingine za kifedha na hali ya mifuko tulileta marekebisho ya sheria hapa na Bunge lako likapitisha kuwa mafao lazima yalipwe ndani ya siku 60,” amesema Katambi.

Kwa upande wa uwajibikaji, Katambi amesema kumekuwa na uwajibikaji mkubwa baada ya kupitishwa sheria kwa kuhakikisha kabla ya miezi mitatu wanahakikisha taarifa za wastaafu.

Amesema kutokana na marekebisho hayo changamoto hiyo imeisha.

Mbunge wa viti maalumu (CCM), Janejelly Ntate amehoji kwa nini upande wa Serikali haujaweka faini wanapochelewesha mafao ya wafanyakazi.

Akijibu swali hilo, Katambi amesema upande wa PSSSF wanalipa asilimia tano kama riba na NSSF wanalipa asilimia 15 na hivyo pande zote mbili kuna riba.

Related Posts