Nyota wa nje walivyopamba kikosi Twiga Stars

Dar es Salaam. Nyota 11 wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania, wameitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ kitakachoingia kambini Februari 9, 2025 kujiandaa na mechi dhidi ya Guinea Ikweta, Februari 20, 2025.

Mechi hiyo ni ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (Wafcon) 2026 zitakazofanyika Morocco.

Benchi la ufundi la Twiga Stars chini ya Bakari Shime limeendelea kutoa fursa kubwa kwa Watanzania wanaocheza soka la kulipwa nje ingawa bado wachezaji wanaocheza Ligi Kuu ya wanawake Tanzania wamezingatiwa katika uteuzi wa kikosi hicho.

Nyota 11 wa kigeni ambao wamejumuishwa katika kikosi cha Twiga Stars na timu zao kwenye mabao ni Noela Luhala (Asa Tel Aviv, Israel), Enekia Kasonga (FC Mazatlan, Mexico), Diana Lucas (Trabzonspor, Uturuki), Hasnath Ubamba (FC Masar,Misri), Maimuna Kaimu (Zed FC, Misri0 Malaika Meena (Bristol City, England), Suzan Adam (Tutankhamun, Misri), Aisha Masaka (Brighton, England), Oppa Clement na Juletha Singano (FC Juarez, Mexico) na Clara Luvanga (Al Nasr, Saudi Arabia).

Hapana shaka tegemeo kubwa la Twiga Stars ni Luvanga anayecheza Al Nasr ya wanawake kutokana na kasi ya kufumania nyavu ambayo amekuwa akiionyesha katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia ambapo hadi sasa amefumania nyavu mara 12.

Ukiondoa Luvanga, kocha Bakari Shime ana wigo mpana wa uteuzi katika eneo la ushambuliaji kwani pia ana Aisha Masaka ambaye amerejea uwanjani katika kikosi cha Brighton kinachoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake England baada ya kuwa nje kwa wiki kadhaa akiuguza majeraha ya mkono.

Lakini pia kuna Oppah Clement ambaye hivi karibuni amejiunga na FC Juarez inayoshiriki Ligi Kuu Mexico akitokea Henan Jianye ya China lakini pia yupo Stumai Abdallah wa JKT Queens ambaye anashika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania akiwa amefumania nyavu mara 11.

Kikosi kinaundwa pia na wachezaji 19 wanaozitumikia timu tofauti zinazoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania ambao ni Najat Abasi, Lidya Maximilian, Donisia Minja, Anastazia Katunzi, Christer Bahera, Joyce Lema, Janeth Christopher, Winifrida Gerard, Jamila Rajab na Stumai Abdallaha wa JKT Queens, Janeth Shija, Vaileth Nicholaus na Aisha Mnunka (Simba), Asha Mrisho (Mashujaa Queens), Ester Maseke (Bunda Queens), Mary Siyame (Fountain Gate) na Asha Ramadhan (Yanga Princess).

Related Posts