Aliyekuwa bosi wa jeshi Rwanda afichua mapya ya Kagame

Dar es Salaam. Wakati Rais wa Rwanda, Paul Kagame akisema hajui kama kuna majeshi ya nchi yake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), aliyekuwa kiongozi wa jeshi la nchi hiyo, Kayumba Nyamwasa amesema hiyo ni hadaa.

Awali, akizungumza katika mahojiano na Kituo cha Televisheni cha CNN jana Jumatatu, Januari 3, 2025, Rais Kagame amesema hafahamu kama majeshi yake yake yapo mashariki mwa DRC.

Kagame alipoulizwa iwapo kuna vikosi vyovyote vya Rwanda nchini DRC alijibu: “Sifahamu.”

Kwa mujibu wa  Umoja wa Mataifa (UN), inakadiriwa wanajeshi kati ya 3,000 hadi 4,000 wa Rwanda wanasimamia na kuwasaidia wapiganaji wa Kundi la M23 mashariki mwa DRC kupambana na vikosi vya Serikali.

Akizungumza na Mtandao wa Extra Africa leo, Fabruari 4, 2025, Nyamwasa aliyewahi kuwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda kabla ya kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini, amesema mara kadhaa Kagame amewahi kukiri kuwepo kwa majeshi ya Rwanda nchini DRC.

“Mara kwa mara nimemsikia Rais Paul Kagame kwenye televisheni akikiri kuwepo kwa majeshi ya Rwanda nchini DRC, anasema kama majeshi yapo huko kwa nini yasiwepo huko? Kwa hiyo hapo amekubali,” amesema.

Nyamwasa aliyewahi pia kuwa Mkuu wa Idara ya Inteljensia ya nchi hiyo, amegusia mkataba wa amani kati ya Rwanda na DRC.

“Mkataba wa amani kati ya Rwanda na DRC unazungumzia kuondoa majeshi, hiyo haimaanishi kwamba yapo kwenye himaya ya Rwanda, bali yapo Congo. Kwa hiyo kama mko pale mnapigana na kuna watu kila mahali, huwezi kusema kuwa hakuna anayekufa.

“Kwa hiyo, unaposema mamia na maelfu ya wanawake na watoto wanakimbia, je wanakimbia kwa sababu kuna mtu amerusha maputo? Hawakimbii maputo au kwa sababu kuna mtu amewapa maua, wanakimbia kwa sababu wanauawa,” amesisitiza.

 “Kwa hiyo kama kuna mtu anapeleka majeshi na watu wanakimbia, halafu tunasema hatufanyi hivi, unaona mabomu, watu wanakimbia, nini maana yake? Tunaona miili ya watu imelala chini wakiwa wameuawa au mtu anasema sio sisi?”

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF), Julius Malema ameitaka Serikali ya Afrika Kusini kuchukua hatua kwa kauli za Rais Kagame kwa nchi hiyo.

Ametoa kauli hiyo kufuatia majibizano kati ya Rais Kagame na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa kuhusu mgogoro wa DRC.

Katika majibizano hayo kupitia mtandao, Rais Kagame alimkosoa Rais Ramaphosa huku akisema nchi yake iko tayari kwa mapambano.

Akizungumza na CNN jana, Rais Kagame alisema Afrika Kusini imepeleka majeshi yake DRC kwa kuwa inanufaika na madini ya nchi hiyo.

Kupitia mtandao wa Youtube, Malema amesema maneno anayotoa Rais Kagame hayamlengi tu Rais Ramaphosa, bali Waafrika Kusini wote.

“Unajua alipokuwa akimsema Rais alikuwa anatusema sisi, hawezi kutueleza sisi kama hivyo, hawezi kuua watu wetu kama hivyo.

“Kuna tatizo kubwa, sisemi kwamba twende tukashambulie, ila nasema tujitoe, tujipange upya na kama Rwanda ina lolote katika hili, tuwafuate kwa sababu hatuwezi kuona Rwanda inatuamrisha na Kagame anatutuelekeza cha kufanya,” amesema.

Amesema suala la Rwanda kuwa na jeshi DRC, halina ubishi, “na Sadc (Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika) imekubali kwamba Jeshi la Rwanda linahusika, nani ni Mkuu wa Jeshi la Rwanda? Ni Kagame.”

Related Posts