Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ameahidi kuendelea kuisaidia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) licha ya wananchi wa Afrika Kusini kutoa wito wa kuondoka Kongo wanajeshi wa nchi hiyo kufuatia vifo vya walinda amani 13 wa Afrika Kusini.
Rais Ramaphosa amebainisha kuwa suala la kufikia amani na usalama wa kudumu mashariki mwa DRC linahitaji utashi wa pamoja wa jamii ya kimataifa. ” Afrika Kusini haitaacha kuwasaidia na kuwaunga mkono watu wa Kongo”, amesema Rais Cyril Ramaphosa.
Amebainisha kuwa, wana wasiwasi kuhusu uvumi unaoendelea kuhusu hali ya wanajeshi wao na hali ya vita nchini DRC. “Wananchi wa Afrika Kusini wanapasa kuwatia moyo na kuwaunga mkono askari wetu jasiri kwa waume ambao wamejitolea maisha yao kwa ajili ya kurejesha amani na utulivu barani Afrika.
“Kuwepo kwa jeshi la Afrika Kusini mashariki mwa Kongo si tangazo la vita dhidi ya nchi au taifa lolote bali ni sehemu ya juhudi za kuleta amani na kuwalinda maelfu ya watu ambao maisha yao yapo hatarini kufuatia hali ya mgogoro inayoisibu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo,” amemalizia kusema Rais wa Afrika Kusini.
Takriban watu 100,000 wamekimbia makazi yao katika mji wa Goma tangu mji huo udhibitiwe na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda ambayo imekanusha madai hayo.