Mpinzani wa Simba CAF kujulikana Qatar

Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limetangaza tarehe ya droo ya robo fainali ya mashindano ya  Klabu Bingwa na Kombe la Shirikisho Afrika kwa timu zilizofuzu hatua hiyo msimu huu ambapo pia limepanga tukio hilo kufanyika Doha, Qatar.

Baada ya kumaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kundi A, la Kombe la Shirikisho Afrika, Simba inatarajia kukutana na timu mojawapo iliyomaliza katika nafasi ya pili kwenye kundi lake ambapo inaweza kukutana na ama Asec Mimosas (Ivory Coast), Stellenbosch (Afrika kusin) na Al Masry (Misri).

Simba ambao ndiyo wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Kimataifa walifanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali baada ya kumaliza nafasi ya kwanza katika kundi A ambapo ilikuwa imepangwa na timu za CS Constantine, CS Sfaxien na Bravos do Maquis ya Angola.

Vijana wa Fadlu Davids walikusanya jumla ya pointi 13 baada ya kushinda mechi nne, sare mechi moja na kupoteza mechi moja katika mechi sita walizocheza.

Timu za Kombe la Shirikisho zilizofuzu robo fainali ni Simba (Tanzania), CS Constantine (Algeria), Stellenbosch (Afrika Kusini), RS Berkane (Morocco), ASEC Mimosas (Ivory Coast), USM Alger (Algeria) na Al Masry pamoja na Zamalek zote za Misri.

Timu za Klabu Bingwa zilizofuzu robo fainali ni Al-Hilal (Sudan), Espérance de Tunis (Tunisia) MC Alger (Algeria) FAR Rabat (Morocco) Al Ahly (Misri) Pyramids (Misri) na Mamelodi Sundowns pamoja na Orlando Pirates zote za Afrika Kusini.

Related Posts