Dar es Salaam. Taasisi ya Gates Foundation, imesema uamuzi wa kumpa Rais Samia Suluhu Hassan tuzo ya Gates Goalkeeper, umetokana na uongozi wake ulivyoonyesha kuguswa na athari za kupuuzwa kwa afya ya uzazi.
Kwa mujibu wa Rais wa Dawati la Usawa wa Jinsia la Gates Foundation Dk Anita Zaidi, uongozi wa Rais Samia Tanzania umepunguza vifo vya wazazi kwa zaidi ya robo tatu na watoto kwa asilimia 80.
Tuzo ya Gates Goalkeeper imeasisiwa na Taasisi ya Bill and Mellinda Gate mwaka 2017 ikilenga kuchochea na kuonyesha juhudi za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) kwa watu mbalimbali.
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva ni miongoni mwa wanasiasa waliowahi kupokea tuzo hiyo mwaka 2024, huku Ursula von der Leyen Rais wa Umoja wa Ulaya akiwa kiongozi mwingine aliyewahi kuipokea.
Tuzo hiyo pia, aliwahi kupewa Waziri Mkuu wa India, Narendra Mondi, kadhalika Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (UN-Women), Phumzile Mlambo-Ngcuka.
Akizungumza katika hafla ya kumkabidhi tuzo hiyo Rais Samia, jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Februari 4, 2025 Dk Anita amesema mkuu huyo wa nchi ameonesha kuguswa na athari za afya ya uzazi.
Amesema ulipofika mwaka 2021, Rais Samia akaapishwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke na ameonyesha anafahamu kwa undani madhara ya kupuuza masuala ya uzazi.
Katika uongozi wake, amesema Serikali ilianza kufanya juhudi mbalimbali ikiwamo kuongeza miundombinu ya uzazi katika vituo vya afya na kutoa suluhisho kwa wazazi.
Amesema ilianzishwa programu ya M-Mama inayosaidia kuwasafirisha wajawazito kwenda vituo vya afya wanapofika siku za kujifungua hasa wale walioko mbali na gari za kubebea wagonjwa.
“Juhudi hizo zilisababisha vifo vya watoto vikapungua zaidi ya robo tatu tangu mwaka 2015 na vifo vya uzazi vimepungua kwa asilimia 80 tangu mwaka 2015, haya ni matokeo makubwa,” amesema.
Amesema mwaka 2015 mataifa mengi duniani yalisaini malengo ya maendeleo endelevu na Tanzania iliahidi kuhakikisha inatoa huduma bora za afya kwa ustawi wa wananchi wake.
“Matokeo ya ahadi hiyo ni kwamba leo hii tunaona kina mama wengi wapo hai wakiendelea kulea watoto wao na watoto wengi wanakuwa wakifurahia na wameepuka vifo,” amesema.
Amesema alianza maisha ya kitaaluma akiwa daktari wa watoto na alishuhudia idadi kubwa ya wanawake wakifariki dunia wakati wa kujifungua.
Katika kipindi hicho, ameeleza alishuhudia watoto wengi wakishindwa kuvuka kipindi cha mwezi mmoja au miwili baada ya kuzaliwa kwao.
Kwa mujibu wa Dk Anita, kwa macho yake aliona madhara ya kupuuzwa kwa afya ya uzazi, watoto wachanga na lishe bora.
Amesema Tanzania ikawa kinara wa umuhimu wa masuala ya unyonyeshaji na imesaidia kukuza lishe za watoto kwa kiwango kikubwa.
Ameeleza tatizo la vichwa vikubwa pia lilipungua baada ya kuzingatiwa kwa matumizi ya Folic Acid.
“Kazi hii inahitaji uongozi bora, ushirikiano na kuweka malengo na makusudi ya kuhakikisha kipaumbele kinawekwa kwenye afya ya uzazi,” amesema.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema tuzo hiyo pamoja na kutambua mchango wa Rais Samia, pia inawahamasisha watendaji wengine kuongeza jitihada za kuboresha maisha ya Watanzania.
“Hakika tuzo hii imetambua safari ya nchi yetu kuelekea katika kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs),” amesema.
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema chini ya uongozi wa Rais Samia kazi kubwa imefanyika katika kuimarisha mifumo ya afya.
Matokeo ya kazi hiyo, amesema ni kuongeza miundombinu ya afya, vikiwemo vituo vya afya, zahanati, hospitali na vifaa vya huduma za afya.
“Hii sio tuzo ya kwanza, kuna nyingine nyingi lakini hii ina upekee kwa ustawi wa maisha ya wanawake wa Tanzania na watoto wote,” amesema Jenista.