Wawili kortini wakidaiwa kumiliki mijusi 226

Dar es Salaam. Wakazi wawili wa Jiji la Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi mbili tofauti za kumiliki mijusi 226 aina ya Coud Gecko yenye thamani ya Sh13.7 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Washtakiwa hao ni mfanyabiashara, Hika Hika (48) maarufu Majoka mkazi wa Mwanagati Wilaya ya Ilala na Shaban Mzomoke (45) maarufu Kisukari na mkazi wa Tandale na fundi randa ambao kwa pamoja wamesomewa mashtaka sita.

Washtakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumanne Februari 4, 2025 na kusomewa kesi mbili za uhujumu uchumi, na wakili wa Serikali, Tumaini Mafuru mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rahim Mushi.

Kabla ya kuwasomea kesi hizo, Hakimu Mushi aliwataka washtakiwa hao kutokujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi isipokuwa kwa kibali maalumu.

Katika kesi ya kwanza, wakili Mafuru amedai kuwa, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2997/2025.

Amedai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2024 na Januari 10, 2025, eneo la Shekilango lililopo wilaya ya Ubungo.

Inadaiwa kuwa, siku hiyo washtakiwa walijihusisha na biashara ya nyara za Serikali ambazo ni mijusi 213 aina ya Coud Gecko yenye thamani ya Sh 13.05 milioni mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.

Shtaka la pili ni kujihusisha na nyara hizo tukio wanalodaiwa kulitenda Januari 10, 2025 eneo la Shekilango.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na mijusi hao bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini Tanzania na la tatu ni kumiliki nyara za Serikali tukio wanalodaiwa kulitenda Januari 10, 2025  eneo la Mwanagati, Wilaya ya Ilala.

Hata hivyo, washtakiwa walishindwa kutimiza masharti ya dhamana ya kila mshtakiwa kuwasilisha Sh3.5 milioni au awe na wadhamini wawili wenye barua kutoka Serikali za Mitaa wenye vitambulisho vinavyotambulika, watakaosaini bondi ya Sh3.5milioni.

Katika kesi ya pili, Wakili Mafuru amedai kuwa, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 2998/2025.

Amewataja washtakiwa hao katika kesi hiyo kuwa ni Shaban Mzomoke na Hika Hika, wanaokabiliwa na mashtaka matatu.

Akiwasomewa mashtaka yao, wakili Mafuru alidai katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2024 na Januari 10, 2025 eneo la Shekilango.

Siku hiyo, washtakiwa hao wanadaiwa kujihusisha na biashara ya mijusi mikubwa 13, ambayo imekufa yenye Sh765, 575 mali ya Serikali.

Shtaka la pili ni kujihusisha na nyara hizo na shtaka la tatu ni kumiliki mijusi hiyo, bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori nchini.

Wakili Mafuru amedai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Kesi hizo mbili zimeahirishwa hadi Februari 17, 2025 kwa ajili ya kutajwa.

Related Posts