VITA ya bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara Yanga na timu inayoshika nafasi ya mwisho kwenye msimamo wa ligi hiyo KenGold, itaamuliwa kibabe kesho kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Saalam.
Wengi wanasubiri kuona beki mkongwe Kelvin Yondani atakavyokuwa na kazi ya kuizuia safu ya ushambuliaji ya Yanga inayoongozwa na Clement Mzize mwenye mabao saba na Prince Dube aliyefunga matano.
Huu ni mchezo wa mzunguko wa 17 katika duru la pili baada ya ule wa kwanza uliochezwa Septemba 25, 2024 Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya kumalizika kwa wageni Yanga kushinda 1-0.
Ugumu wa mchezo huo unatokana na mabadiliko ya vikosi vya timu zote mbili, wakati zinakutana duru la kwanza, Yanga ilikuwa inafundishwa na Miguel Gamondi lakini sasa nafasi yake imechukuliwa na Sead Ramovic.
Kwa upande wa KenGold alikuwepo Jumanne Challe akisimama kama kaimu kocha mkuu baada ya kuondoka Fikiri Elias. Kwa sasa timu hiyo inafundishwa na Mserbia, Vladislav Heric na huu utakuwa mchezo wake wa kwanza wa ligi tangu akabidhiwe kikosi hicho.
Safu ya ulinzi ya KenGold imeimarishwa kwa kiasi fulani baada ya mechi 16 zilizopita kuruhusu mabao 29, yakiwa ni mengi zaidi kuliko timu zote zinazoshiriki ligi hiyo.
Katika kuboresha safu hiyo ya ulinzi, KenGold imetumia vizuri dirisha dogo la usajili ikimshusha beki mkongwe, Kelvin Yondani aliyewahi kucheza Simba na Yanga kwa mafanikio makubwa.
Ukongwe wake unaweza kuwa na faida kwenye kikosi cha KenGold ambacho pia kimejiimarisha maeneo mengine kama vile kuinasa saini ya Obrey Chirwa na Zawadi Mauya waliowahi kuitumikia Yanga, pia wanaye Bernard Morrison, ambaye kesho hatacheza kwa sababu anauguza majeraha.
Nyota wengine wapya wa KenGold waliosajiliwa dirisha dogo lililofungwa Januari 15, 2025 baadhi yao ni Erick Kabamba, Kiala Lassa na Sadala Lipangile.
Kocha Msaidizi wa KenGold, Omary Kapilima, amesema: “Tumejiandaa vizuri kuikabili Yanga, tunaiheshimu ni timu kubwa lakini tunataka matokeo mazuri katika mchezo wa kesho.
“Ni kweli tumeingiza majina mengi mapya, mwanzo tulikuwa na changamoto katika eneo la ulinzi lakini sasa tumeleta wachezaji wazoefu, nina imani kesho tutakuwa na mchezo mzuri na kupata alama tatu.”
Uwepo wa Yondani ambaye amekabidhiwa kitambaa cha unahodha, unaweza kumlinda vizuri kipa wa kikosi hicho, Castor Mhagama na dhahama ya ukali wa safu ya ushambuliaji ya Yanga.
Yanga inayoongoza kwa kufunga mabao mengi (34) kwenye ligi msimu huu, mechi sita ambazo Kocha Ramovic ameisimamia timu hiyo na kushinda zote, ameshuhudia vijana wake wakitikisa nyavu mara 22 na kuruhusu mawili pekee.
Katika mabao hayo 22 yaliyofungwa mechi sita zilizopita, Mzize na Dube kila mmoja ana matano, huku Pacome Zouzoua akiwa na manne, Kennedy Musonda, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ na Mudathir Yahya wakifunga mawili.
Mwingine ni kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz KI aliyefunga moja, lingine kati ya hayo 22 ni la kujifunga kutoka kwa beki wa Fountain Gate, Jackson Shiga.
KenGold ambayo huu ni msimu wa kwanza kushiriki Ligi Kuu Bara, hii itakuwa ni mara ya pili kucheza dhidi ya Yanga baada ya duru la kwanza kupoteza nyumbani kwa bao 1-0. Hata hivyo, Ramovic anaamini KenGold itaingia tofauti katika mchezo wa kesho kutokana na mabadiliko yaliyofanyika katika kikosi chao.
“Tutakutana na timu ambayo imepata wachezaji wengi wapya. Pia kocha ana aina yake ya uchezaji. Itakuwa ngumu sana kwa sababu hatujui wanachezaje.
“Lakini labda kama tulivyokutana na wapinzani wetu wa mwisho, wataenda kwenye mfumo wa kuzuia zaidi, hivyo inamaanisha lazima tutengeneze nafasi kutafuta maeneo ya kupita, lazima tujaribu kucheza kwenye nusu yao. Yote kwa yote, utakuwa mchezo mgumu tena sana, Lakini, kama ninavyosema siku zote, sisi ni timu bora zaidi Tanzania.
“Tunajiamini sana, lakini pia tunaheshimu kila timu tunayocheza nayo, tunataka kuipa kila timu heshima inayostahili, hivi ndivyo tunavyofanya siku zote.
“Tumeshinda taji mara tatu mfululizo, na tunataka kushinda tena. Ikiwa tunataka kufanya tena hivyo, tunahitaji kushinda mchezo huu kwa sababu ni mchezo muhimu sana kwetu. Hilo ndilo lengo letu.
“Tangu nimefika tuliboresha katika maeneo mengi na ukweli ni kwamba tunapaswa kuwa bora zaidi eneo la umaliziaji. Katika mchezo uliopita (dhidi ya Kagera Sugar) licha ya kwamba tulifunga mabao mengi (4-0) lakini pia tulipata nafasi nyingi mbele ya goli.”
Kuhusu uwezekano wa winga mpya wa kikosi hicho, Jonathan Ikangalombo maarufu Ikanga Speed kucheza kesho, Ramovic amefichua bado hajawa fiti.
“Jonathan ni mchezaji mzuri, lakini hayuko fiti. Hayuko tayari kucheza lakini unaweza kuona ana ubora mkubwa. Atatusaidia sana. Jambo la kwanza tunachopaswa kufanya ni kumweka katika levo nzuri ambayo tunaitaka, hatutaki acheze kipindi hiki akiwa hayupo fiti ili kumuepusha na majeraha kwani atatakiwa kukimbia kwa kasi.
“Lakini bila shaka ni mchezaji mzuri na katika siku chache zijazo atatusaidia sana.”
Kocha Msaidizi wa KenGOld, Omary Kapilima amezungumzia hali ya kikosi chake akisema: “Wachezaji wote wapo sawa sawa kasoro Bernard Morrison ambaye ana changamoto, anamalizia matibabu ili aanze mazoezi, lakini waliobaki wote wapo vizuri.
“Katika mechi 16 tumepata alama sita, baada ya ligi kusimama, hivyo ni kama tunaanza upya kesho tukitegemea kupata alama tatu.”
Kabla ya mchezo huo wa saa 10 jioni, mapema saa 8:00 mchana Tabora United itaikaribisha Namungo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.
Rekodi zinaonyesha timu hizo mara ya mwisho zilikutana Agosti 25, 2024 kwenye Dimba la Majaliwa mkoani Lindi na wenyeji Namungo walikubali kichapo cha mabao 2-1. Kabla ya hapo, msimu uliopita Namungo ilishinda 3-2 kisha sare ya 1-1. Upinzani wa timu hizo unaonekana ni mkubwa sana na zinapokutana kila moja lazima ifunge bao.
Kocha wa Namungo, Juma Mgunda ana kazi ya kuwaongoza vijana wake na mechi tatu za mwisho ugenini katika ligi hawajapoteza wakishinda mbili na sare moja wakati Tabora United ya Mkongomani Anicet Kiazayidi mechi tatu za mwisho nyumbani imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja ya juzi dhidi ya Simba. kesho wana kazi ya kujiuliza tena.