KAMPASI YA MIZENGO PINDA, KATAVI, KUPANUA WIGO WA KUONGEZA UDAHILI WA WANAFUNZI

Kampasi ya Mizengo Pinda mkoani Katavi na mojawapo ya Kampasi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo inaenda kupanua wigo wa kitaaluma kwa kuongeza idadi ya wanafunzi kufuatia mapitio mapya ya programu yanayoendelea chuoni kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambapo idadi ya wanafunzi itaongezeka.

Kuongezeka kwa wigo wa wanafunzi kumeelezwa na Kaimu Rasi wa Ndaki hiyo Prof. Anna Sikira wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mpimbwe na viunga vyake kupitia Kituo cha Redio cha Mpimbwe FM ambapo amesema serikali imetenga fedha za kuboresha miundombinu ya Kampasi ambapo kukamilika kwake kutapelekea idadi ya wanafunzi wanaojiunga na SUA kupitia hiyo Kampasi kuongezeka suala linaloenda sambamba na kuongezeka kwa kozi zitakazofundishwa.

Prof. Sikira amesema ongezeko hilo linatija kwa wananchi wa Katavi kwani wataweza kupata elimu bora inayoendana na shughuli wanazozifanya jambo litakaloongeza thamani kiuchumi kupitia shughuli hizo ikiwemo kilimo na urinaji wa asali.

“Saizi tunategemea mabadiliko makubwa ya hii Kampasi yetu hapa, linajengwa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi takribani 400 kwa wakati mmoja pia tunajenga jengo la kisasa la taaluma ambapo kukamilika kwake ina maanisha hata madhari ya hii Kampasi itakuwa nzuri”, alisema Prof. Sikira ambaye pia alielezea historia ya Chuo.

Mkuu wa Idara ya Sayansi Kilimo Bw. Joseph Ruboha amewahimiza wananchi wa Mpimbwe kutumia fursa ya uwepo wa Kampasi hiyo kupata uzoefu kwa kutembelea na kujifunza namna bora ya utengenezaji mizinga, urinaji wa asali na shughuli nyingine za kilimo, akisema SUA imejikita katika kutafuta suluhu ya changamoto za wakulima nchini.

Kwa upande wake, Afisa Mipango katika Kampasi ya hiyo Bw. Rasuli Kalokola amesema wamepanga kujenga kiwanda kidogo ya uchakataji wa asali kitakachotumika kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi pamoja na utoaji wa elimu ya uchakataji wa kisasa kwa wakulima wa asali katika mkoa wa Katavi na mikoa ya jirani.

Bw. Kalokola ameongeza kuwa wamepanga kujenga kiwanda cha mbao ambacho kitatumika kwa ajili ya mafunzo ya wanafunzi ya utengenezaji mizinga ya kisasa, ambapo mradi huo umefadhiliwa na Mfuko wa Misitu Tanzania (TAF) wenye thamani ya shilingi milioni mia moja.

Related Posts