WAFANYABIASHARA wawili wakazi wa jijini Dar es Salaam wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kesi mbili za uhujumu uchumi kwa kukutwa na nyara za serikali ambazo ni Mijusi 226
Imedaiwa kati ya hao Mijusi 13 ni wakubwa na Mijusi aina Coud Grecko 213 walio hai.
Katika hati ya mashtaka iliyosomwa mahakamani hapo na wakili wa serikali Mwandamizi Tumaini Mafuru imewataja washtakiwa hao kuwa Shaban Mzomoka maaruufu kwa jina la Kisukari (45) mkazi wa Tandale na Hika Shaban Hika maarufu kama Majoka (48) anayeishi Mwanagati.
Katika kesi ya kwanza imedaiwa Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rahim Mushi kuwa katika tarehe tofauti kati ya Novemba 2024 na Januari 10,2025 washtakiwa hao waliongoza genge la uhalifu ambapo ni kujihusisha na biashara ya nyara za serikali ambazo ni mijusi 13 wenye thamani ya Usd 325 sawa na Tsh 796,575 bila ya kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori. mali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
Washtakiwa hao wanadaiwa pia katika kipindii hicho hicho walikutwa wakijihusisha na nyara hizo za serikali ambazo ni Mijusi hao 13.
Mafuru amedai kuwa kati ya Januari 10,2025 huko Shekilango katika Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam washtakiwa walikutwa wakiwa na Nyara za serikali ambazo ni mijusi 13 wenye thamani ya USD 325 sawa na TSh. 796,575 mali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, washtakiwa walikutwa na nyara hizo bila ya kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa wanyamapori.
Hata hivyo washtakiwa wamekana mashtaka hayo na wameachiwa huru kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili wenye barua.
Katika kesi ya pili inadaiwa kati ya Novemba 2024 na Januari 10, 2025 huko Shekilango Wilayani Ubungo Dar es Salaam, washtakiwa waliongoza genge la uhalifu ambapo ni kujihusisha na biashara ya nyara za serikali (Mijusi 213 waliokuwa hai).
Pia washtakiwa wanadaiwa kujihusisha na nyara za serikali ambapo Januari 10,2025 huko Mwanagati ndani ya Wilaya ya Ilala, washtakiwa walipokea viumbe hai ambavyo ni Mijusi aina ya Coud Grecko wenye thamani ya USD 5325 sawa na Tsh. 13,051,575.
Washtakiwa pia wanadaiwa siku na mahali hapo hapo walikutwa wakimiliki Mijusi hiyo 213 bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa wanyamapori mali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo washtakiwa wamerudishwa rumande hadi Februari 17,2025 baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyowataka kuweka fedha taslimu Sh. Milioni tatu na nusu au kuwa na wadhamini wawili kila mmoja.
Kwa mujibu upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haujakamilika.