Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amepokewa na wakazi wa Dodoma baada ya kutunukiwa tuzo ya Gates Goalkeeper huku akisema tuzo hiyo ni ya wahudumu wa sekta ya afya na Watanzania wote.
Tuzo ya Gates Goalkeeper, imeasisiwa na Taasisi ya Bill and Mellinda Gates mwaka 2017 ikilenga kuchochea na kuonyesha juhudi za utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs) kwa watu mbalimbali.
Rais wa Brazil, Luiz Inácio Lula da Silva ni miongoni mwa wanasiasa waliowahi kupokea tuzo hiyo mwaka 2024, huku Ursula von der Leyen Rais wa Umoja wa Ulaya akiwa kiongozi mwingine aliyewahi kuipokea.
Tuzo hiyo pia, aliwahi kupewa Waziri Mkuu wa India, Narendra Mondi, kadhalika Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake (UN-Women), Phumzile Mlambo-Ngcuka.
Rais Samia amepokewa leo Jumanne Februari 4, 2025, katika Uwanja wa Ndege Dodoma akitokea jijini Dar es Salaam alipopatiwa tuzo hiyo mapema asubuhi.
Wakazi wa jijini la Dodoma waliokuwa na mabango ya kumpongeza kwa kupata tuzo hiyo walijipanga katika barabara inayoelekea uwanja wa ndege huku wakiimba nyimbo za kumsifia.
Baadhi ya mabango hayo yaliyokuwa na picha ya Rais Samia yalikuwa yameandikwa hongera bimkubwa, tulilolitaka wajumbe wamelifanya mwaka 2025 ni wako mama, kazi umemaliza hatudai tunakuahidi ushindi wa kishindo.
Akiondoka katika uwanja huo, Rais Samia alipanda katika gari la wazi akiwapungua wakazi hao huku mkono mmoja ukiwa ameshika tuzo hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kushuka katika uwanja huo, Rais Samia amesema tuzo hiyo ina maana kubwa kwa sababu anadhani dunia imefahamu juhudi za Tanzania katika huduma za afya.
“Sio tu huduma za afya kwa jumla ila huduma za kiafya kwa mama na mtoto. Kama mnavyojua miaka minne vifo vya kina mama wakati wa kujifungua vilikuwa vinafikia 566 kwa kina mama 100,000 wanaojifungua,”amesema.
Hata hivyo, amesema wamefanya uwekezaji mkubwa katika kujenga majengo, kununua vifaa, uwekezaji kwenye kusomesha madaktari na kuajiri wafanyakazi wa afya ya msingi.
Amesema uwekezaji huo umeweza kupunguza vifo vya kina mama na watoto kutoka 556 hadi 104 wakati wa kujifungua, lakini lengo waliloagizwa na dunia ni inapofika 2030 wafikie vifo 70 tu.
“Sasa tuko 104 hakika ikifika mwaka 2030 tutafikia lengo ama tutapita kidogo kwa sababu jitihada zinaendelea. Lakini kwa watoto chini ya miaka mitano tumepunguza kwa kiasi kikubwa,” amesema.
“Lakini tunakazi kubwa ya kufanya kwa watoto wanaozaliwa ambao tulikuwa tunawapoteza kwa sababu kadhaa, wakati mwingine kina mama wanatumia dawa za kienyeji, wakati mwingine wanachelewa kufika hospitali lakini hatukuwa na vifaa vya kuokoa maisha yao,” amesema.
Amesema sasa wamevinunua na kuwa tuzo hiyo, siyo ya Rais ila ni ya wahudumu wote wa sekta ya afya.
“Kuanzia madaktari, ma-specialist (madaktari bingwa), wauguzi na wote wanaotoa huduma hadi wafanyakazi wa ngazi ya jamii hii ndio tuzo yao ni tuzo ya Taifa ni tuzo ya sekta ya afya. Ina umuhimu mkubwa sana. Tunashukuru kwamba sisi Tanzania ndio Taifa la mwanzo la Afrika kupewa tuzo hii,” amesema.
Amesema ni kwa jitihada kubwa walizoweka katika sekta ya afya ndizo zilizofanyikisha kupata tuzo hiyo.
“Kila jambo lazima kuwa na utashi wa kisiasa. Kwa hiyo kiongozi akiwa na utashi wa kisiasa wa kufanya jambo hakika linakuwa. Kwa hiyo nakubali nimeipokea kwa ajili yangu na Watanzania wote,” amesema.
Mkazi wa Mailimbili, Scolastica Mtui amesema wamekuja kumpongeza Rais Samia kwa kupunguza vifo vya wanawake wakati wa kujifungua, jambo ni matokeo makubwa ya uwekezaji katika sekta ya afya.
“Hapo awali, mtu ulikuwa unaogopa kubebea ujauzito, ukiona takwimu zinazotolewa unaahirisha, lakini hivi sasa ametusaidia kwa kusogeza huduma karibu na wananchi,”amesema.
Msanii wa mama ongea na mwanao, Mwanaheri Hamad amesema Rais Samia licha ya kufanya vyema katika sekta ya afya, amekuwa Rais wa kwanza kwa kufanya filamu ambayo imefundisha mambo mengi na pia kuwapeleka Korea wasanii kujifunza masuala ya sanaa.
Mkazi wa Nkhungu, Mwira Khatibu amesema Rais Samia amekuwa na uongozi mzuri kwa kuwasaidia wanawake katika mambo mbalimbali ikiwamo mikopo ambayo amesema hivi sasa iko nje kwa nje.