Leo, Februari 5, 2025, niko tena jijini Dodoma kushuhudia Chama cha Mapinduzi (CCM) kikitimiza miaka 48 ya uwepo wake na miaka 48 ya kushika dola. Siri kuu ya mafanikio ya miaka hiyo, ni Watanzania kuichagua mwaka hadi mwaka na kwa vile huu ni mwaka wa uchaguzi, nimeona hakuna ubaya kuwaelimisha watu kuhusu siri ya mafanikio ya CCM kwa miaka 48, kwa kuwaelimisha kuhusu malengo yake, nguvu yake na mabadiliko gani lazima iyafanye.
CCM ilianzishwa kwa azimio la mkutano mkuu wa Taifa wa pamoja wa TANU na ASP, jukumu lao ni kuimarisha umoja, kuleta mapinduzi ya kijamaa Tanzania na kuendeleza mapambano ya ukombozi katika Afrika na kote duniani kwa kuzingatia na kuthamini kazi nzuri ya kimapinduzi ziliyofanywa na vyama hivyo katika kuondoa unyonyaji na kudharauliwa na kumfikisha kwenye uhuru na kuheshimiwa.
Hivyo, CCM kikazaliwa Februari 5, 1977 na makao makuu yake yako Dodoma. Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar iko Unguja na kuna Ofisi Ndogo ya Makao Makuu Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Imani ya CCM ni: “Binadamu Wote ni Sawa”. Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake na “Ujamaa na Kujitegemea” ambayo ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru.
CCM ina malengo 19, lengo kuu likiwa ni kushinda katika uchaguzi wa Serikali Kuu na serikali za mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na serikali za mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa pili.
Pia, inalenga kulinda na kudumisha uhuru wa nchi. Kwenye hili, CCM imefanikiwa sana, kwa sababu ndiyo imekuwa inashinda chaguzi zote bara na visiwani. Malengo mengine ni kulinda na kudumisha uhuru wa nchi yetu na raia wake, hili CCM imefanikiwa sana.
Lengo la kuhimiza ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea kwa mujibu wa Azimio la Arusha, inabidi libadilishwe, kwa sababu Azimio la Arusha, limebadilishwa na Azimio la Zanzibar, Tanzania sasa haifuati siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, tunafuata siasa ya uchumi wa soko.
Kuona kwamba kila mtu anayo haki ya kupata kutoka katika jamii hifadhi ya maisha yake na mali yake kwa mujibu wa sheria, hili linakwenda vizuri.
Mengine ni kuona kwamba katika nchi yetu, kila mtu aliye na uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi; na kazi maana yake ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu riziki yake, linakwenda vizuri.
Kusimamia haki na maendeleo ya wakulima, wafanyakazi na wananchi wengine wenye shughuli halali za kujitegemea; na hasa kuona kwamba kila mtu ana haki ya kupata malipo yanayostahili kutokana na kazi yake linakwenda vizuri.
Mengine ni kuona kwamba kwa kutumia vikao vilivyowekwa, raia anayo haki ya kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi wa mambo ya Taifa na yanayomhusu na kwamba anao uhuru wa kutoa mawazo yake wa kwenda anakotaka, wa kuamini dini anayotaka na kukutana na watu wengine, ili mradi havunji sheria au taratibu zilizowekwa, hili linatekelezwa.
Hili la nchi yetu kutawaliwa kwa misingi ya kidemokrasia ya kijamaa inabidi libadilike, kwa sababu demokrasia ya kijamaa ni demokrasia ya chama kimoja tu cha siasa kama China. Tanzania sasa ni nchi ya vyama vingi, hili lazima libadilike na CCM kama chama tawala, ndiye chama mlezi wa vyama vingine vyote.
Sote tulishuhudia Tundu Lissu wa Chadema alipopigwa risasi, Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais, alikwenda kumtembelea hospitalini Nairobi na akiwa Rais, alikwenda kumtembelea nchini Ubelgiji.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alikabiliwa na kesi mbaya ya ugaidi, Rais Samia akaingilia kati, akafanya mazungumzo ya mwafaka na kumwachia Mbowe ambapo alikwenda Ikulu kumshukuru na kumlilia shida, Rais Samia alimsikiliza, ndio sasa tumeiona Chadema hii iliyofufuka, hata Lissu kama mwenyekiti mpya wa Chadema, Rais Samia amemwalika, wasemezane. Hili jukuma la CCM kuwa mlezi wa vyama liendelezwe, lakini vyama navyo viungane, huu utitiri wa vyama hauna maslahi mema kwa mustakabali wa upinzani imara.
CCM inaendelea kufanya vema kwenye kuhifadhi, kukuza na kudumisha imani na moyo wa kimapinduzi miongoni mwa Watanzania pamoja na ushirikiano na wanamapinduzi wenzetu.
CCM inaendelea kudumisha heshima ya binadamu kwa kufuata Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu.
Hili la dola inakuwa mhimili wa uchumi wa Taifa inabidi libadilike, sasa sekta binafsi ndiyo inapaswa kuwa mhimili na jukumu la dola ni kuweka mazingira wezeshi, kama kinachofanyika kwenye PPP.
Hili la shughuli za ushirika liendelee ila siyo ushirika wa ujamaa, bali ushirika wa kisasa na shughuli nyinginezo halali za wananchi za kujitegemea na kuona kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya wananchi
Na hasa jitihada za kuondosha umasikini, ujinga na maradhi. Hongera CCM kwa kutimiza miaka 48.