Madiwani Handeni Mjini waagiza ofisi ya ardhi ifungwe siku 14

Handeni. Baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji wa Handeni, mkoani Tanga limeazimia na kumuagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuifunga kwa siku 14 ofisi ya ofisa ardhi kwa kushindwa kutatua migogoro ya viwanja.

Akizungumza kwenye kikao cha kawaida cha baraza hilo kilichofanyika leo Jumanne Februari 4, 2025 mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mussa Mkombati amesema kuna mgogoro wa ardhi, eneo la kitalu A, Kata ya Kwenjugo ambao viongozi mbalimbali waliagiza ufanyiwe kazi, lakini hakuna utekelezaji uliofanyika.

Amesema mgogoro unatokana na halmashauri kuchukua viwanja vya wananchi kwa makubaliano kuwa watafidiwa, lakini hawakufidiwa badala yake wamepewa watu wengine ambao wameendeleza ardhi hiyo licha ya kuwepo mgogoro.

Mkombati amesema zimeshatolewa hati tatu kwa wamiliki wengine wa viwanja hali inayochochea tatizo hilo, hivyo wamekubaliana kuifunga ofisi ya ardhi hadi atakapofika Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi kutatua tatizo hilo.

Amesema ofisi ya mkuu wa wilaya, Chama cha Mapinduzi (CCM) na baraza walishatoa mwongozo wa jinsi ya kutatua mgogoro huo, lakini ofisi ya ardhi haijatekeleza maagizo hayo bali imeendelea na mchakato wa kugawa viwanja kwa watu wengine na kutoa hati za umiliki.

“Baraza limejiridhisha pasipo shaka kwamba hoja zilizotolewa na diwani wa Kata ya Kwenjugo, Twaha Mgaya na kwa kauli moja baraza linakuelekeza mkurugenzi kufunga ofisi za watu wa ardhi kwenye Halmashauri ya Mji wa Handeni.

“Hii itasaidia viongozi wetu kuja kuona shida ya mgogoro huu na wautatue kiutalaamu,” amesema.

Awali, akizungumzia mgogoro huo, diwani Mgaya amesema mwaka 2004 walianza mchakato wa kupima viwanja vya wananchi bure wakilenga baada ya kukamilika watalipa fedha ya upimaji na kwamba, walishaanza kulipia.

Amesema katika eneo la kitalu A wapo wananchi walioshindwa kulipa, hivyo halmashauri kupitia idara ya ardhi ilichukua viwanja hivyo kwa makubaliano kuwa watawalipa fidia wananchi ya asilimia 40 baada ya kuviuza lakini hilo halikufanyika badala yake wakapewa wengine.

Viwanja 580 vimehusika katika mgogoro huo baada ya wahusika kushindwa kulipia upimaji ambao gharama ni Sh120,000 kwa kila kiwanja.

Kutokana na hilo, wananchi waliokuwa wakimiliki viwanja hivyo, awali walitaka warudishiwe viwanja au walipwe fidia hivyo kuibuka mgogoro kati ya wamiliki wa awali, wa sasa na halmashauri.

Mwenyekiti wa Mipango Miji wa Halmashauri ya Mji Handeni, Siri John amesema wamefikia hatua ya kufunga ofisi kwa sababu baadhi ya wananchi wametamka kwamba watafanya lolote lile kurudisha maeneo yao, hivyo kuna hatari ya kutokea machafuko.

Related Posts